Hali si shwari Bahrain baada ya kuhujumiwa nyumba ya Sheikh Qassim
Hali nchini Bahrain leo imeripotiwa kuwa mbaya siku moja baada wanajeshi wa ufalme wa Aal Khalifa kuvamia nyumba ya mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Sheikh Isa Qassim na kuua wafuasi wake kadhaa.
Siku ya Jumanne, wanajeshi wa Bahrain walivunja mlango wa nyumba ya Sheikh Qassim katika kijiji cha DIraz na kuwaua watu wasiopungua watano na kuwajeruhi wengine wengi.
Milio ya risasi ilisikika huku wanajeshi wakitumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanaya waandamanaji waliokuwa na hasira. Aidha hadi sasa watu 286 wamekamatwa huku maafisa 19 wa jeshi wakijeruhiwa katika ghasia hizo.
Maandamano yanaripotiwa kuendelea katika eneo hilo huku wasiwasi ukitanda kote Bahrain.
Sheikh Qassim, kiongozi wa kiroho wa chama cha Kiislamu cha Al Wefaq yuko katika kifungo cha nyumbani baada ya kupokonywa uraia mwezi Juni mwaka jana.
Aidha Jumapili alihukumiwa kifungo cha nyumbani cha mwaka moja kwa kosa la kukusanya Khums huku utawala ukichukua udhibiti wa mali za Waislamu zenye thamani ya dola milioni nane ambazo alikuwa akizisimamia. Leo wabunge nchini Iran wametoa taarifa na kulaana utawala wa Aal Khalifa nchini Bahrain kwa kumkandamiza Sheikh Qassim. Aidha wabunge wa Iran wamesema hatua zilizochukuliwa na utawala wa kifalme Bahrain ni dhidi ya dini na dhidi ya binadamu.