Mateka 60 wa Kipalestina waliogoma kula wahamishiwa hospitalini
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i29572-mateka_60_wa_kipalestina_waliogoma_kula_wahamishiwa_hospitalini
Mateka wasiopungua 60 wa Kipalestina miongoni mwa maelfu ya wafungwa hao waliosusia kula chakula katika magereza ya utawala wa Kizayuni wa Israel wamehamishiwa hospitalini baada ya hali zao kuzidi kuwa mbaya.
(last modified 2026-05-06T11:35:21+00:00 )
May 25, 2017 03:21 UTC
  • Mateka 60 wa Kipalestina waliogoma kula wahamishiwa hospitalini

Mateka wasiopungua 60 wa Kipalestina miongoni mwa maelfu ya wafungwa hao waliosusia kula chakula katika magereza ya utawala wa Kizayuni wa Israel wamehamishiwa hospitalini baada ya hali zao kuzidi kuwa mbaya.

Mawakili wa jumuiya ya kutetea mateka wa Kipalestina ambao wamekutana na Wapalestina waliosusia kula katika jela ya Israel ya kuogofya ya Ohali Kidar wametangaza kuwa hali za kifaya za wafungwa wengi ni mbaya sana na kwamba baada ya kugoma kula kwa muda wa siku 38 wanapaswa kuhamishiwa hospitalini.

 Kwa mujibu wa mawakili hao, kutokana na kudhoofu kimwili kupita kiasi, baadhi ya wafungwa hao hawawezi hata kuvaa nguo zao wenyewe.

Tangu tarehe 17 ya mwezi uliopita wa Aprili, mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa kwenye magereza ya utawala wa Kizayuni wa Israel wameanzisha mgomo usio na mpaka wa kususia kula kutokana na kupuuzwa haki zao za kibinadamu katika magereza hayo.

Marwan Al-Barghuthi

Pendekezo la kuanzisha mgomo wa kususia kula lilitolewa na Marwan Al-Barghuthi, mjumbe wa kamati kuu ya harakati ya Al-Fat'h, Ahmad Saadat, Katibu Mkuu wa Harakati ya Wananchi wa Palestina pamoja na viongozi wengine kadhaa wa wafungwa hao wanaoshikiliwa kidhulma kwenye jela za utawala haramu wa Israel.

Awali idadi ya wafungwa waliosusia kula ilikuwa 700, lakini baada ya muda, malalamiko dhidi ya hali mbaya waliyonayo wafungwa hao na kutoshughulikiwa hali zao za kiafya pamoja na haki zao yalishamiri, ambapo kwa sasa idadi ya wafungwa Waplaestina waliosusia kula imefikia 2,000.

Kuna Wapalestina wapatao 5,000 wanaoshikiliwa kwenye jela za utawala wa Kizayuni wa Israel, ambapo 62 miongoni mwao ni wanawake na wengine 300 ni watoto, ambao kisheria hawastahili kufungwa jela.../