Wazayuni waitaka Marekani iendelee kuliunga mkono kundi la Daesh (ISIS)
Baadhi ya maafisa wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel wameishauri Marekani kuwa haipasi kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) litokomezwe kwa sababu kundi hilo halijawahi kuwa tishio na hatari kwa Israel.
Katika makala iliyoandikwa na Zuhair Andraos kwenye gazeti la Al Ra'ayul-Yaum linalochapishwa London, Uingereza mwandishi huyo ameeleza kuwa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh halijafanya shambulio lolote la kijeshi dhidi ya Israel au kulenga maslahi ya Israel na wazayuni ndani na nje ya mipaka ya utawala huo haramu.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, hivi karibuni aliyekuwa Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni wa Israel Moshe Ya'alon alifichua kuwa magaidi wa kundi la ukufurishaji la Daesh waliwahi mara moja kuwashambulia kimakosa askari wa utawala huo katika eneo la miinuko ya Golan kusini mwa Syria lakini waliomba radhi haraka.
Wakati huo huo gazeti la kila wiki la POLITICO linaochapishwa nchini Marekani limeeleza katika ripoti yake kuwa waandishi wa gazeti hilo wamefanya mahojiano kadhaa na maafisa waandamizi wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel na kwamba maafisa hao wametahadharisha kuhusu mkakati wa kulisambaratisha moja kwa moja kundi la Daesh wakisisitiza kuwa hatua hiyo haitakuwa na tija nyengine zaidi ya majuto.
Tangu kujitokeza makundi ya kigaidi likiwemo la kitakfiri la Daesh (ISIS) katika eneo la Mashariki ya Kati, utawala wa Kizayuni umekuwa mmoja wa waungaji mkono wakuu wa makundi hayo. Duru za habari zimewahi kutangaza kuwa utawala huo haramu umewahamishia kwenye ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu (Israel) na kuwapatia matibabu magaidi wa kundi la Daesh waliojeruhiwa vitani nchini Syria.../