UN: Matatizo yote ya Wapalestina yanatokana na Israel
Umoja wa Mataifa umesema kuwa, matatizo yote waliyo nayo Wapalestina hivi sasa yanatokana na kukaliwa kwa mabavu ardhi zao na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Shirika la habari la AFP jana Jumatano lilinukuu taarifa ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA na kuandika kuwa, ukosefu wa amani, mashambulizi na ukandamizaji wa wanajeshi wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina ndiko kulikoongeza kiwango kikubwa cha wakimbizi wa Palestina na uvunjaji wa haki za binadamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwaka 2016 eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan lilikuwa na wakimbizi milioni moja na laki sita kutokana na Israel kuwavunjia nyumba zao. Kati ya wakimbizi hao, 750 walikuwa ni watoto wadogo. Ongezeko hilo kubwa la wakimbizi wa Palestina halijawahi kushuhudiwa mfano wake tangu mwaka 2009.
Si hayo tu, lakini pia walowezi wa Kizayuni wanawazuia mamia ya Wapalestina kutoka katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kwa ajili ya kwenda kutafuta mahitaji yao muhimu na ya lazima, yakiwemo madawa ya kutibu wagonjwa wao.
Kwenye Ukanda wa Ghaza pia, mgogoro wa kibinadamu unakuwa mkubwa siku baada ya siku. Kutokana na kuzingirwa kila upande na Israel kwa miaka kumi sasa, ukanda huo umekuwa na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira duniani.