Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran: Taasisi za kimataifa ni washirika katika jinai za utawala wa Kizayuni
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa taasisi za kimataifa zinashiriki katika jinai za utawala wa Kizayuni.
Mohammad Reza Aref ameeleza haya katika radiamali yake kufuatia shambulio la kikatili la Israel katika shule ya wakimbizi wa Kipalestina katika kitongoji cha al Daraj mashariki mwa mji wa Gaza.
Wakimbizi zaidi ya mia moja wameuawa shahidi katika hujuma hiyo ya kikatili ya utawala haramu wa Israel. Mohammad Reza Aref amesema maafa makubwa ya binadamu yaliyotokea huko Gaza ni dhihirisho jingine la ukiukaji wa kihistoria wa haki za taifa madhulumu la Palestina na vitendo vya utumiaji mabavu vya wazi dhidi ya wamiliki wa asili wa ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Kizayuni.
Aref ameongeza kuwa, taasisi za kimataifa na wale wanaodai kutetea haki za binadamu ulimwenguni ambao wamenyamaza kimya ni washiriki wa jinai hizo za kinyama.
Jeshi la utawala wa Israel unaotekeleza mauaji ya kimbari jana Jumamosi uliwashambulia Wapalestina waliokuwa katika swala ya alfajiri katika shule ya al-Tabi’in katika kitongoji cha al Daraj katika mji wa Gaza. Wapalestina wasiopungua 100 wameuawa shahidi na wengine wengi kujeruhiwa. Wapalestina karibu 200 walikuwa wakiswali swala ya alfajiri jana walipokabiliwa na shambulio la anga la jeshi la utawala wa Kizayuni.