UNHCR: Idadi ya wakimbizi duniani imeongezeka na kufika milioni 120
(last modified Fri, 14 Jun 2024 07:11:22 GMT )
Jun 14, 2024 07:11 UTC
  • UNHCR: Idadi ya wakimbizi duniani imeongezeka na kufika milioni 120

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetangaza kuwa, idadi ya wakimbizi duniani imefikia milioni 120.

Hayo yamo katika ripoti ya kila mwaka ya UNHCR ambayo imeeleza kuwa, vita vya Gaza, Sudan na Myanmar vimechangia pakubwa kuongeza idadi ya watu waliolazimika kukimbia makazi yao kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) amesema kuwa, vita bado ni kichocheo kikuu cha watu wengi kulazimika kuhama makazi yao.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa, mwishoni mwa mwaka jana (2023), watu milioni 117.3 walikimbia makazi yao. Hii ni karibu milioni 10 zaidi ya mwaka mmoja mapema. Aidha kuna karibu mara tatu ya watu wengi waliokimbia makazi yao kwa kulazimishwa kuliko mwaka wa 2012.

Grandi amesisitiza kuwa, kuna ongezeko kubwa la migogoro na mabadiliko ya hali ya hewa ambavyo vinavyochochea zaidi mizozo duniani kote. Mwaka jana, UNHCR ilitangaza dharura 43 katika nchi 29, zaidi ya mara nne kuliko jinsi ilivyokuwa miaka michache iliyopita.

Kadhalika ripoti hiyo inabainisha kwamba, vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini Sudan tangu mwezi wa Aprili 2023 vimesababisha zaidi ya watu wengine milioni tisa kuyahama makazi yao, na kuwaacha karibu Wasudan milioni 11 kukabiliwa na majanga mbalimbali mwishoni mwa mwaka 2023.

Katika Ukanda wa Gaza, Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa watu milioni 1.7 - 75% ya idadi ya watu wamekimbia makazi yao tangu vita vilivyoanzishwa na Israel kulipiza kisasi shambulio la Hamas kwenye ardhi yake mnamo mwezi Oktoba 7.

Kuhusu viita vya Ukraine,  karibu watu 750,000 walikuwa wakimbizi wapya wa ndani nchini humo mwaka jana, na jumla ya wakimbizi wa ndani milioni 3.7 waliorodheshwa mwishoni mwa mwaka 2023. Syria inasalia kuwa na mzozo mkubwa zaidi wa wakimbizi duniani.

Tags