Uhajiri wa kuihama Israel; jinamizi linalousokota utawala haramu wa Kizayuni
Wizara ya Kuvutia Uhajiri ya utawala wa Kizayuni wa Israel, imeonyesha wasi wasi wake mkubwa juu ya kushadidi wimbi la uhajiri kutoka ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, linalohusisha Mayahudi hasa wenye asili ya Russia.
Sambamba na kutangaza takwimu mpya, wizara hiyo imetoa ripoti ikisema kuwa, katika kipindi cha miaka 14 iliyopita, jumla ya walowezi wa Kiyahudi laki mbili na elfu 90 na 300, wamehama Israel na kwenda maeneo mbalimbali ya dunia. Kadhalika Wizara ya Kuvutia Uhajiri ya utawala wa Kizayuni wa Israel, imetangaza kuwa katika kipindi cha miaka hiyo 14, asilimia 38 ya Mayahudi wote waliozihama ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na kwenda sehemu nyingine za dunia walikuwa ni Mayahudi wa Russia. Inafaa kueleza kuwa, vizuizi vya kiidara, mipaka ya kidini na ya masuala ya kiserikali hususan kuhusiana na kadhia ya ndoa, mila na desturi za uzikaji maiti pamoja na hali mbaya ya kimaisha, vimewafanya Warusi hao wakabiliwe na ubaguzi na kukosa haki zao katika ngazi rasmi na za kijamii; na mambo hayo ndizo sababu kuu za kuihama Israel na kutokuwa na hamu tena ya kurejea huko.
Kwa hakika uhajiri wa Mayahudi kuelekea ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ni moja ya stratijia na msingi wa uwepo wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Ilikuwai imetarajiwa kuwa, katika ardhi hizo za Palestina zinazoitwa eti 'ardhi iliyoahidiwa' ambazo zimepatikana kupitia uvamizi na ukaliaji mabavu, Mayahudi hao wahajiri wasingekumbwa na matatizo kama ya ukosefu wa ajira, usalama na umasikini, na hivyo kuandaliwa mazingira mazuri ya uwekezaji, kupata elimu bora na hali ya juu ya ustawi wa jamii bila ya kukbailiwa na ubaguzi wowote. Hata hivyo kinyume na matarajio hayo, wahajiri wa Kiyahudi ambao kwa kuahidiwa na viongozi wa utawala wa Kizayuni kwamba wangeipata pepo iliyoahidiwa huko Palestina, walibaini mara baada ya kuwasili huko kuwepo kwa ubaguzi mkubwa baina ya Wazayuni na hali mbaya ya kisiasa, kiusalama, kijamii na kiuchumi inayotawala ndani ya jamii ya Kizayuni. Israel ni utawala bandia na pandikizi ambao daima umekuwa ukikabiliwa na matatizo makubwa ya muundo wa idadi ya watu na ardhi ambayo ndiyo mambo mawili yanayounda dola na taifa la watu.
Kwa sababu hiyo Israel imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali kuwavutia wahajiri wa Kiyahudi kutoka maeneo tofauti ya dunia ambao tab'an wana hali na asili tofauti ili kwenda kuishi huko katika ardhi za Palestina inazozikalia kwa mabavu. Kwa upande wa kijamii, ni kwamba jamii ya Kizayuni ambayo imeunda utawala wa Kizayuni kupitia wahajiri wa Kiyahudi, ni jamii ambayo haina utambulisho na yenye mpasuko. Ni jamii yenye mgongano ambayo haiwezi kudumu kutokana na mivutano mingi inayotawala ndani yake. Kiujumla ni kwamba kuwepo jamii ya namna hiyo kwa utawala huo bandia wa Kizayuni sambamba na kugubikwa na ubaguzi dhidi ya wahajiri wa Kiyahudi, ni kati ya masuala ambayo yamezidisha malalamiko makubwa kwa watu hao ambao eti wanaitwa raia wa Israel.
Mbali na hayo, Israel inaundwa na jamii ya kimatabaka ambayo yenyewe ni dhihirisho la ubaguzi mkubwa wa rangi; mfano hai zaidi wa suala hilo ukiwa ni ubaguzi wa hali ya juu na miamala miovu na isiyo ya kibinaadamu inaowafanyia Wapalestina katika ardhi zao ulizozitwaa kwa mabavu. Miamala ya kibaguzi ya Kizayuni haiwalengi Wapalestina peke yao, bali inawaandama hata wahajiri wa Kiyahudi waliohamia katika ardhi hizo za Wapalestina. Hatua ya kuwagawa Mayahudi wanaotoka nchi za Magharibi 'Ashkenazi' ambao wanahesabika kuwa watu wa daraja la kwanza na Mayahudi wa Mashariki, ambao wanahesabiwa kuwa watu wa daraja la pili, inabainisha kiwango cha juu cha ubaguzi unaofanywa na utawala huo wa Kizayuni wa Israel. Miamala hiyo ya kibaguzi ndio ambayo imeweka wazi kwamba jamii ya Kizayuni inakabiliwa na tatizo kubwa la kijamii linalotokana na muundo wa kimatabaka unaotawala ndani ya Israel.
Alaa kullihal, hakika ya kile kinachoitwa 'pepo iliyoahidiwa' na utawala wa Kizayuni kwa ajili ya Mayahudi, ni jehanamu ambayo inawafanya Mayahudi hao wazitoroke ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu; ambapo kushadidi kwa hali hiyo ni jinamizi linalowaandama viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusiana na mustakbali wa giza totoro unaoukabili utawala huo haramu.../