Wapalestina wengine watatu wauliwa shahidi Al-Khalil
(last modified Mon, 14 Mar 2016 16:19:37 GMT )
Mar 14, 2016 16:19 UTC
  • Wapalestina wengine watatu wauliwa shahidi Al-Khalil

Askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamewaua shahidi kwa kuwapiga risasi vijana watatu wa Kipalestina karibu na mji wa Al-Khalil katika Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan.

Duru za utawala wa Kizayuni zimedai kuwa askari wa Kizayuni waliwapiga risasi vijana hao wa Kipalestina baada ya vijana hao kuwajeruhi wazayuni wawili.

Mbali na vijana hao watatu waliouliwa shahidi leo asubuhi, siku ya Jumamosi pia Wapalestina wawili akiwemo mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 10 waliuawa shahidi katika shambulio la anga lililofanywa na jeshi la utawala haramu wa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Na hii ni katika hali ambayo mashambulio ya anga ya jeshi la utawala wa Kizayuni yamekiuka makubaliano ya usitishaji vita yaliyofikiwa baina ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS na utawala wa Kizayuni baada ya vita vya siku 50 vya mwaka 2014 vilivyoanzishwa na utawala huo ghasibu dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Tangu mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka uliopita wa 2015 hadi sasa maeneo mbalimbali ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu yamekuwa yakishuhudia wimbi la malalamiko ya upinzani dhidi ya siasa za kichokozi za utawala wa Kizayuni na njama za utawala huo za kupotosha utambulisho wa Baitul Muqaddas pamoja na mpango wake wa kuugawa kiwakati na kimahali msikiti mtukufu wa Al-Aqsa. Wimbi hilo la malalamiko limekuwa maarufu kwa jina la Intifadha ya Quds.

Wapalestina zaidi 200 wameshauawa shahidi tangu ilipoanza Intifadha ya Quds mwezi Oktoba mwaka jana hadi hivi sasa.../

Tags