Qatar yawasilisha rasmi malalamiko UN kutokana na uhasama wa Saudia
Serikali ya Qatar imewasilisha malalamiko yake rasmi kwa Umoja wa Mataifa kufuatia hatua ya Saudia, Bahrain, Misri na Imarat ya kuiwekea mzingiro wa kiuchumi na kisiasa, baada ya nchi hizo kudai kuwa, Doha inaunga mkono ugaidi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Mohammed bin Abdulrahman Al Thani amewasilisha barua mbili kwa nyakati tofauti kwa António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Zeid Ra'ad Al Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa akilalamikia hatua ya nchi hizo kuiwekea mzingiro wa kisiasa na kiuchumi nchi ya Qatar.
Kufuatia hatua hiyo, Saif Bin Ahmed Al Thani, Mkuu wa Idara ya Habari ya serikali ya Qatar sambamba na kuzikosoa serikali za Misri, Saudia, Imarat na Bahrain amesema kuwa, hivi sasa nchi hizo zimeanzisha kampeni kali yenye lengo la kuchafua sura ya serikali ya Doha.
Nchi hizo zilitangaza kukata mahusiano yao na Qatar hapo tarehe tano mwezi huu, sambamba na kuzishawishi nchi mbalimbali kuungana nazo katika kukata mahusiano yao na Qatar.
Tuhuma zilizotumiwa na mataifa hayo dhidi ya Doha ni kwamba nchi hiyo inaunga mkono ugaidi, madai ambayo yamekuwa yakikanushwa na serikali ya Qatar.