Ndege za Israel zawavurumishia mabomu Wapalestina Ukanda wa Ghaza
Ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel zimevurumisha makombora kadhaa katika Ukanda wa Ghaza wakati Wapalestina katika eneo hilo wakiwa wanasherehekea siku kuu ya Idul Fitr.
Taarifa zinasema, mapema leo Jumanne, ndege za kivita za Israel zimevurumisha makombora Ghaza kwa madai ya kulenga vituo vya Brigedi ya Ezzedin Qassam, tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas.
Hujuma hizo zimetekelezwa katika maeneo ya kati, magharibi na kusini mwa Ukanda wa Ghaza. Aidha mashamba ya Wapalestina mashariki mwa Ghaza pia yamekumbwa na hujuma ya mashambulizi ya mizinga ya jeshi la utawala haramu wa Israel.
Wakuu wa utawala wa Tel Aviv wanadai wametekeleza hujuma hizo kwa sababu kulirushwa maroketi kutoka Ukanda wa Ghaza kuelekea eneo lisilo na wakazi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.
Utawala haramu wa Israel mara kwa mara hutekeleza mashambulizi katika Ukanda wa Ghaza huku raia wakiwa ni walengwa wakuu wa mashambulizi hayo.
Utawala haramu wa Israel umetekeleza mashambulizi kadhaa dhidi ya Ukanda wa Ghaza ambapo shambulizi kubwa la mwisho lilikuwa mwezi Julai mwaka 2014. Hujuma hiyo ya wiki kadhaa ilimalizika mwishoni mwa mwezi Agosti ambapo Wapalestina 2,200 waliuawa shahidi wengi wakiwa ni raia wa kawaiada hasa wanawake na watoto.
Aidha Ukanda wa Gaza umekuwa katika mzingiro wa kibaguzi na kidhalimu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, tokea mwaka 2007.