Israel; hatari kuu ya ulimwengu wa Kiislamu
Naibu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu wa Kishia nchini Lebanon amesema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel ndiyo hatari kuu kwa umma wa Kiislamu na kwamba kitendo cha baadhi ya nchi za Kiislamu cha kuwa na uhusiano na Israel ni hatari kubwa kwa Waislamu.
Baadhi ya nchi za Kiarabu hususan Saudi Arabia zimo katika mchakato wa kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Kizayuni na hivi sasa viongozi wa Saudia wanazihesabu harakati za Kiislamu zinazopambana na Israel kama vile Hamas kuwa ndiye adui yao mkubwa.
Kwa mujibu wa shirika la habari la RASA, Sheikh Ali al Khatib alisema hayo jana (Jumatano) na kusisitiza kuwa, jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Waislamu ziko wazi kabisa na hazifichiki. Ameongeza kuwa, utawala wa Kizayuni hadi hivi sasa unaendelea kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina hususan mji wa Quds wenye Kibla cha Kwanza cha Waislamu kama ambavyo pia umewafanya wakimbizi mamia ya maelfu ya Wapalestina.
Naibu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu wa Kishia nchini Lebanon ameongeza kuwa, licha ya kwamba Wapalestina wanaishi katika mazingira magumu mno, lakini hadi leo hii wamekataa kabisa kudhalilishwa, na wamesimama imara katika muqawama wa kupigania ukombozi wa ardhi na haki zao.
Vile vile amesisitizia wajibu wa kuelekezwa nguvu za umma wa Kiislamu kwenye mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni na magenge ya wakufurishaji na kuongeza kuwa: Leo hii zile nchi ambazo zilihusika katika kuundwa magenge ya kigaidi au zilizokuwa zinayaunga mkono makundi hayo katili, zimeanza kujuta na kubadilisha siasa zao.