Mgomo wa kula wa wafungwa wa kisiasa nchini Bahrain
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i31426-mgomo_wa_kula_wa_wafungwa_wa_kisiasa_nchini_bahrain
Wafungwa wa kisiasa nchini Bahrain wanaoshikiliwa katika jela za kutisha za al Jau na al Hawd al Jaf nchini humo wameamua kuanzisha mgomo wa kutokula chochote ikiwa ni kulalamikia dhulma wanayofanyiwa na watawala madikteta wa nchi hiyo.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jul 06, 2017 23:17 UTC
  • Mgomo wa kula wa wafungwa wa kisiasa nchini Bahrain

Wafungwa wa kisiasa nchini Bahrain wanaoshikiliwa katika jela za kutisha za al Jau na al Hawd al Jaf nchini humo wameamua kuanzisha mgomo wa kutokula chochote ikiwa ni kulalamikia dhulma wanayofanyiwa na watawala madikteta wa nchi hiyo.

Wafungwa wa kisiasa nchini Bahrain wanafanyiwa mateso na miamala mibaya sana na ya kila siku katika jela za utawala wa Aal Khalifa na wananyimwa haki zao za kimsingi kabisa. Mgomo wa chakula wa wafungwa wa kisiasa nchini Bahrain unaofanyika kwa jina la "haki zilizoporwa" bila ya shaka yoyote unafanyika kutokana na siasa zilizo dhidi ya ubinadamu za utawala wa kiimla wa Aal Khalifa ambao umewapora wananchi wa Bahrain haki zao za kimsingi kabisa. Bahrain hivi sasa imo katika orodha ya nchi zinazofanya ukandamizaji mkubwa mno wa haki za binadamu duniani na walimwengu hivi sasa wanafuatilia kwa wasiwasi mkubwa ukandamizaji usiosita wanaofanyiwa wananchi wasio na ulinzi wa Bahrain. 

Baadhi ya picha za watoto na vijana wadogo waliofungwa jela nchini Bahrain

 

Kwa kweli hakuna siku yoyote iendayo kwa Mungu bila ya kuwa shahidi wa ukandamizaji mkubwa wa ukoo wa Aal Khalifa dhidi ya wapinzani wa utawala huo wa kifalme. Hii ni katika hali ambayo wapinzani wengi wa utawala huo wa kiimla baada ya kutekwa nyara na mamluki wa ukoo wa kifalme hupotezwa na wasijulikane waliko. Ni jambo lisilo na shaka kwamba, mazingira yanayotawala nchini Bahrain hivi sasa ni ya ukandamizaji wa kuchupa mipaka huku askari wa ukoo wa Aal Khalifa wakiendeeza siasa za kipolisi katika kona zote za kisiwa hicho ili kuwanyamazisha wapinzani. 

Mtaalamu wa masuala ya kisiasa Ralph Schoenman wa nchini Marekani anasema: "Suala la kukandamizwa na kunyanyaswa wapinzani nchini Bahrain ni mwendo wa kendelea na ni jambo la kila siku. Kwa kushirikiana na vikosi vya kijeshi vya Saudi Arabia, askari wa Bahrain wameamua kushambulia jamii nzima ya Mashia wa nchi hiyo na kunyamazisha sauti yoyote ya demokrasia nchini humo. Vitendo vya utawala wa Bahrain dhidi ya wapinzani vinaonesha sura halisi ya utawala huo ya kukanyaga haki za kimsingi kabisa na haki za kidimokrasia za wananchi wa nchi hiyo."

Kwa kweli, utawala wa kiimla wa Aal Khalifa unatumia hila na ulaghai wa kila namna na hasa siasa za kueneza chuki za kimadhehebu ili kuhakikisha unaendelea kubakia madarakani kwa gharama yoyote ile. Hata hivyo nukta ya kutiliwa maanani hapa ni mwamko wa wananchi wa Bahrain mbele ya utawala kandamizi wa Aal Khalifa. Mwamko huo umefelisha njama zote zinazojaribu kuzima sauti ya ukombozi wa haki za wananchi hao. Katika miaka ya hivi karibuni maeneo mbalimbali ya Bahrain yamekuwa yakishuhudia maandamano ya takriban kila siku ya wananchi wanaopigania haki zao. Kwa kweli, ukandamizaji nchini Bahrain ni mkubwa kiasi kwamba licha ya nchi hiyo kuwa na idadi ndogo ya raia, lakini ni moja ya nchi zenye wafungwa wengi zaidi wa kisiasa duniani. Jela za nchi hiyo hivi sasa zimejaa kupindukia wafungwa wa kisiasa. 

Wanajeshi wa ukoo wa kifalme wa Bahrain wakikandamiza raia

 

Tangu tarehe 14 Februari 2011, wananchi wa Bahrain walianzisha mapambano ya kupigania haki zao za kimsingi walizoporwa na ukoo wa Aal Khalifa. Matakwa makuu ya wananchi wa Bahrain ni kuwa na serikali ya kisheria na viongozi wanaochaguliwa na wananchi, kukomeshwa ubaguzi, kuweko uhuru wa kisiasa na kuheshimiwa uadilifu, haki za binadamu, uhuru na kutokubali kuwa kibaraka wa Magharibi. Hata hivyo kwa msaada wa kila upande wa Saudi Arabia na baadhi ya tawala zisizo za kidemokrasia za Kiarabu, ukoo wa Aal Khalifa umekuwa muda wote huu ukifanya ukandamizaji mkubwa dhidi ya raia wa Bahrain. 

Amma cha kusikitisha zaidi ni kuona kuwa jamii ya kimataifa haichukui hatua yoyote ya maana ya kuwaokoa wananchi wa Bahrain mbele ya ukandamizaji wa kutisha wanaofanyiwa. Hali ya wafungwa wa kisiasa katika jela za nchi hiyo ni mbaya mno kiasi kwamba sasa wafungwa hao wamelazimika kuanzisha mgomo wa kutokula chakula kwa matumaini ya kufikisha kilio chao kwa wapenda haki duniani.