HAMAS: Iran inaendelea kuunga mkono mapambano ya Palestina
Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea kuunga mkono mapambano ya wananchi wa Palestina na hakuna wakati ambao Tehran ilisitisha himaya na uungaji mkono wake huo.
Fawzi Barhoum amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na Shirika la Habari la Mehr la Iran na kusisitiza kwamba, himaya na uungaji mkono wa Iran kwa wananchi madhulumu wa Palestina ungali unaendelea na Hamas inapongeza na kuthamini misaada inayotolewa na Tehran kwa ajili ya mapambano ya wananchi wa Palestina.
Barhoum amesema kuwa, Hamas ikiwa moja ya harakati za wananchi inahitajia himaya kubwa na ya kila upande ili iweze kuendelea na harakati zake za kukabiliana na utawala haramu wa Israel unaotenda jinai kila uchao dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.
Akizungumzia azimio la hivi karibvuni la Kamati ya Utendaji ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Utamaduni na Sayansi UNESCO ambalo liliulaani utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kukiuka sheria za kimataifa katika mji wa Quds (Jerusalem) na Ukanda wa Gaza na kueleza kwamba, mji wa Quds hauna uhusiano wowote na Wazayuni, msemaji huyo wa Hamas amebainisha kwamba, azimio hilo limefichua uongo wa makumi ya miaka wa Wazayuni.
Ameongeza kuwa, kutajwa mji wa Quds kwamba, ni mji unaojkaliwa kwa mabavu kunahesabiwa kuwa ni hatua moja mbele na muhimu kwa taifa la Palestina na vilevile nchi za Kiarabu na Kiislamu.