Hizbullah: Israel itashtushwa mno na uwezo wetu wa kijeshi iwapo itatuchokoza
Mkuu wa Baraza la Utendaji la Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah nchini Lebanon, amesema kuwa, iwapo utawala wa Kizayuni utaanzisha vita vyovyote dhidi ya harakati hiyo, Tel Aviv itashangazwa na uwezo mkubwa wa kijeshi wa wanamapambano wa Hizbullah.
Sayydi Hashim Safiyud-Din ameyasema hayo katika mahojiano na televisheni ya al Manar ya Lebanon kwa mnasaba wa mwaka wa 11 wa vita vya siku 33 vilivyopiganwa wakati wa msimu wa joto mwaka 2006 na kusisitiza kuwa, Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah haijiandai kuanzisha vita vyovyote, lakini ikiwa itachokozwa, bila ya shaka itamshangaa adui kwa mbinu mpya zinazojulikana na zisizojulikana.
Akibainisha kwamba hii leo uwezo wa muqawama katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali kwa moyo wa kujitolea umeongezeka mno na kwamba Hizbullah ipo katika mazingira mazuri sana na kwamba hali hiyo itaendelea kwa kipindi chote ambacho taifa la Lebanon litaendelea kushirikiana na harakati hiyo ya Kiislamu. Ameongeza kuwa, ingawa ni kweli kwamba hivi sasa harakati hiyo imepata zana mpya za kisasa za kijeshi, lakini ripoti zinazotolewa na utawala wa Kizayuni kuhusu uwezo wa kijeshi wa harakati hiyo si usahihi, kwani taasisi za intelejensia na upelelezi za adui huyo haziwezi kufahamu uhalisia wa mambo juu ya zana na silaha za kijeshi za Hizbullah.
Tarehe 12 Julai hadi 14 Agosti mwaka 2006, utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu, nchi za Ulaya na Marekani, ulifanya mashambulizi makali kwa muda wa siku 33 dhidi ya wananchi wa Lebanon. Hata hivyo utawala huo ulipata pigo kubwa kwa kushindwa vibaya na wanamapambano wa Hizbullah na hivyo kuamua kukimbia.