Wanajeshi Wazayuni wamkamata Mufti wa Quds
Wanajeshi dhalimu wa utawala wa Kizayuni unaoikalia kwa mabavu Quds tukufu jana walimkamata Mufti wa mji huyo, Sheikh Muhammad Hussein mara baada ya Sala ya Ijumaa nje ya Masjidul Aqswa.
Televisheni ya al Alam imemnukuu "Sheikh Khalid Hamu" aliyekuwa pamoja na Mufti Muhammd Hussein akisema kuwa, kwanza wanajeshi wa utawala wa Kizayuni walifunga eneo la kuingilia kwenye msikiti huo na Waislamu wakalazimika kusali kwenye eneo la al Asbat, mbele ya msikiti wa al Aqswa. Wanajeshi hao makatili hawakutosheka na hilo, bali wamemkamata Mufti wa Quds ikiwa ni ushahidi wa wazi kuwa, hawakutaka Waislamu watekeleze kabisa ibada ya Sala ya Ijumaa hiyo jana.
Jihad Hussein, mwana wa kiume wa Mufti wa Quds amesema kuwa, jana vijana wa Palestina walifanya operesheni ya kupambana na Wazayuni, hivyo wanajeshi wa Israel waliamua kumalizia hasira zao kwa kumkamata mwanachuoni huyo ambaye hadi tunaandaa habari hii ilikuwa haijajulikana amepelekwa wapi.
Mapema jana asubuhi, vijana wa Palestina walipambana na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni katika uwanja wa Msikiti wa Aqsa. Vijana watatu wa Palestina wameuawa shahidi na wanajeshi wawili Wazayuni wameangamizwa. Mwanajeshi mwengine mmoja wa Israel amejeruhiwa kwenye mapigano hayo.
Zaidi ya Wapalestina 330 wameshauliwa shahidi kwa kupigwa risasi na wanajeshi katili wa Israel na wengine zaidi ya 2400 wameshajeruhiwa tangu ilipoanza Intifadha ya Quds mwezi Oktoba 2015 hadi hivi sasa.