Arab League: Israel inacheza na moto kuhusu kadhia ya Quds
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i32162-arab_league_israel_inacheza_na_moto_kuhusu_kadhia_ya_quds
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imeutahadharisha utawala wa Kizayuni wa Israel kwamba 'unacheza na moto' kutokana na kushadidisha ukandamizaji dhidi ya Wapalestina wa Quds Tukufu inayokaliwa kwa mabavu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 23, 2017 09:41 UTC
  • Arab League: Israel inacheza na moto kuhusu kadhia ya Quds

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imeutahadharisha utawala wa Kizayuni wa Israel kwamba 'unacheza na moto' kutokana na kushadidisha ukandamizaji dhidi ya Wapalestina wa Quds Tukufu inayokaliwa kwa mabavu.

Taarifa ya Arab League iliyotolewa leo Jumapili na Ahmed Aboul Gheit, Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo imesema kadhia ya Quds ni mstari mwekundu ambao Waislamu na Waarabu kote uliwenguni katu hawawezi kuiruhusu Israel kuukanyaga.

Sambamba na kuashiria kuwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu itafanya mkutano wa dharura Jumatano ijayo mjini Cairo Misri kuhusu kadhia ya Quds, taarifa hiyo imesisitiza kuwa, utawala haramu wa Israel unachochea mgogoro mkubwa ambao hauwezi kuuzima kati yake na nchi za Kiarabu na ulimwengu wa Kiislamu.

Tangu tarehe 14 Julai mwaka huu, Israel imeshadidisha siasa zake za ukandamizaji dhidi ya Wapalestina katika Msikiti wa al-Aqsa, ambapo hadi sasa Wapalestina watano wameuawa shahidi na makumi ya wengine kujeruhiwa.

Wanajeshi katili wa Israel wakiwashambulia Waislamu nje ya Msitiki wa al-Aqsa

Hii ni katika hali ambayo, António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza wasiwasi wake kuhusu ukatili na hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuwazuia Wapalestina kutekeleza ibada ya Swala ndani ya Msikiti wa al-Aqsa, katika mji huo unaokaliwa kwa mabavu wa Quds (Jerusalem).

Wakati huo huo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kufanya kikao kesho Jumatatu kujadili kadhia hiyo ya Quds, kutokana na ombi la Misri, Ufaransa na Sweden.