Qatar: Saudia inaendesha kisiasa Ibada ya Hijja
(last modified Sun, 30 Jul 2017 15:13:44 GMT )
Jul 30, 2017 15:13 UTC
  • Qatar: Saudia inaendesha kisiasa Ibada ya Hijja

Kamisheni Taifa ya Haki za Binadamu nchini Qatar imelalamikia vikali uendeshaji wa kisiasa wa ibada tukufu ya Hijja unaofanywa na utawala wa Aal-Saud wa Saudi Arabia.

Taarifa ya kamisheni hiyo imesema kwamba, Riyadh imewawekea vikwazo na vizingiti chungu nzima Mahujaji wa Qatar wanaotaka kwenda kutekeleza ibada hiyo muhimu ya Uislamu.

Baadhi ya vizingiti hivyo ni kuwalazimisha raia wa Qatar walioko nje ya nchi kurejea nchini ili wasafiri kuelekea Saudi Arabia kutekeleza Hijja. Kadhalika raia wa Qatar wanaotaka kwenda kuhijji mwaka huu watalazimika kuondokea katika viwanja viwili vya ndege pekee vilivyoko Doha.

Maiti za Mahujaji waliokufa kutokana na usimamizi mbaya wa Hijja Septemba 2015

Kamisheni Taifa ya Haki za Binadamu ya Qatar imewasilisha malalamiko hayo kwa Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayesimamia masuala ya haki ya kuabudu ikisisitiza kuwa kitendo hicho cha utawala wa kifalme wa Aal-Saudi kinakiuka sheria na makubaliano ya kimataifa yanayomdhaminia kila mtu uhuru wa kuabudu.

Kamisheni hiyo imesema ni jambo la kushangaza namna Saudia, ambayo pamoja na nchi tatu za Kiarabu wapambe wake ilikata uhusiano wa kidiplomasia na Qatar kwa tuhuma bandia za kuunga mkono ugaidi; inavyotumia na kuendesha ibada hiyo tukufu kisiasa.

Huko nyuma Saudi Arabia imewahi kutumia ibada hiyo kisiasa dhidi ya Mahujaji wa Kiirani na Yemen. 

 

Tags