Bashar Assad: Syria inakabiliwa na ugaidi hatari
Rais wa Syria amesema kuwa, nchi hiyo inakabiliwa na ugaidi ambao hauna kifani katika historia ya sasa katika upande wa ukubwa wake, chuki na ukatili wake.
Rais Bashar Assad wa Syria ameyasema hayo kwa mnasaba wa maadhimisho ya mwaka wa 72 tangu kuundwe jeshi la nchi hiyo na kuongeza kuwa, magaidi wa kitakfiri wa Daesh ni maadui wa kihistoria wa nchi hiyo ambao wanafanya jitihada za kudhibiti nchi mbalimbali kwa msaada wa nchi za kanda hii na za nje ya Mashariki ya Kati.
Ameashiria mafanikio makubwa ya nchi yake yaliyotokana na mapambano na kusimama kidete taifa la Syria na kusema: Jeshi na taifa la Syria linaendelea kupata mafanikio kutokana na kusimama kidete, kushirikiana na wananchi na damu za watu waliosabilia nafsi kwa ajili ya nchi yao.

Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 baada ya makundi ya kigaidi kama Daesh na Jabhatu Nusra kuvamia ardhi ya nchi hiyo yakisaidiwa na nchi kama Marekani, Saudi Arabia, Uturuki, Umoja wa Falme za Kiarabu na utawala haramu wa Israel.