Wazayuni waandamana kulalamikia ufisadi wa Netanyahu
Mamia ya Wazayuni wamefanya maandamano katika mji wa Petah Tikva dhidi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu anayeandamwa na tuhuma za ufisadi.
Wazayuni hao waliandamana jana jioni nje ya makazi ya Avichai Mandelblit, Mwanasheria Mkuu wa Israel, wakimtuhumu kuwa anamkingia kifua Netanyahu kwa kuendesha kesi za ufisadi dhidi yake kwa mwendo wa kinyonga.
Mwezi Machi mwaka huu, polisi ya Israel kwa mara nyingine tena ilimhoji Netanyahu; hiyo ikiwa ni mara ya nne ndani ya mwezi mmoja kumsaili kuhusu kesi ya kupokea rushwa inayomkabili yeye na mke wake.
Netanyahu na mkewe wanatuhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa baadhi ya mashirika makubwa ya kibiashara na vilevile kufanya mazungumzo na Arnon Mozes, mchapishaji na mmiliki mwenza wa gazeti la Yediot Ahronoth ili atangaze habari zinazompendelea kwa lengo la kulidhoofisha jarida pinzani la Israel, la Hayom.
Kabla ya kukabiliwa na kesi hii, Benjamin Netanyahu alishawahi kuhojiwa mara tatu huko nyuma kuhusu ufisadi wa fedha na kutumia vibaya madaraka.
Ufisadi umekuwa jambo la kawaida katika utawala wa Kizayuni wa Israel na katika fremu hiyo, Ehud Olmert, Waziri Mkuu wa zamani wa utawala huo hivi sasa amefungwa jela kutokana na ubadhirifu wa fedha.