Vyumba vya mauti nchini Bahrain na kushadidi uteswaji wa wapinzani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i33538-vyumba_vya_mauti_nchini_bahrain_na_kushadidi_uteswaji_wa_wapinzani
Makundi matatu ya haki za binaadamu ya 'Taasisi ya Haki ya Kidemokrasia na Haki za Binadamu' 'Jumuiya ya Haki za Binaadamu nchini Bahrain' na 'Amani kwa ajili ya Demokrasia na Haki za Binaadamu' yametoa ripoti na kusema kuwa, utawala wa kifalme wa Aal-Khalifa umekuwa kila mara ukikandamiza maandamano ya amani ya wananchi na kuwatesa wapinzani.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Aug 23, 2017 22:03 UTC
  • Vyumba vya mauti nchini Bahrain na kushadidi uteswaji wa wapinzani

Makundi matatu ya haki za binaadamu ya 'Taasisi ya Haki ya Kidemokrasia na Haki za Binadamu' 'Jumuiya ya Haki za Binaadamu nchini Bahrain' na 'Amani kwa ajili ya Demokrasia na Haki za Binaadamu' yametoa ripoti na kusema kuwa, utawala wa kifalme wa Aal-Khalifa umekuwa kila mara ukikandamiza maandamano ya amani ya wananchi na kuwatesa wapinzani.

Ripoti iliyotolewa na makundi hayo chini ya anwani inayosema, 'Vyumba vya Mauaji' imesema kuwa, waandamanaji na wapinzani nchini Bahrain wanaoshikiliwa kwenye jela na mahabusu rasmi na za siri za utawala wa Aal Khalifa katika vituo vya wazi na vya siri wanafikwa na mateso ya kutisha ya maafisa usalama wa utawala huo. Aidha ripoti zilizotolewa kuhusiana na jela wanakoshikiliwa wanaharakati wa kisiasa nchini humo zinaelezea uwepo wa hali mbaya sana inayotawala katika korokoro hizo na akthari ya ripoti hizo zinafananisha jela za utawala wa Aal-Khalifa na jela za enzi za utawala wa Manazi nchini Ujerumani. Ripoti hizo zimebainisha kuwa akthari ya askari wa jela za utawala wa Aal Khalifa wameletwa kutoka nje ya nchi hiyo na kwamba jela hizo zina ratiba maalumu za kutisha na kuogofya zinazotekelezwa kwa ajili ya kuwatesa mahabusu.

Maandamano ya amani ya raia wa Bahrain

Katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni ukandamizaji wa utawala wa Aal-Khalifa uliongezeka zaidi nchini Bahrain. Kwa mujibu wa ripoti za mashirika ya haki za binaadamu, Bahrain ambayo ni moja ya nchi ndogo sana za Kiarabu katika eneo la Magharibi ya Asia, inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wafungwa wa kisiasa. Hadi sasa zaidi ya wafungwa wa kisiasa elfu 10 wanaendelea kushikiliwa katika jela za utawala wa nchi hiyo ambapo 150 kati yao wamefungwa vifungo vya maisha. Aidha watoto 150 ni kati ya watu wanaoshikiliwa kisiasa huku raia 200 wengine wakiwa wamepoteza viungo vyao vya mwili kutokana na utesaji wa kutisha wa maafisa usalama wa Bahrain. Kituo cha haki za binadamu nchini Bahrain pia kimetangaza kuwa, kimepata nyaraka za kuaminika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani zinazoonyesha kuwa wizara hiyo imetoa kozi maalumu za mafunzo kwa wafanyakazi wa vyombo vya intelijinsia na upelelezi vya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Bahrain. 

Kamatakamata inayofanywa na Aal-Khalifa dhidi ya wanaharakati wa kisiasa

Scott Rickard mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa nchini Marekani anazungumzia suala hilo kwa kusema: "Mahusiano ya kiintelejinsia na kisiasa yaliyopo kati ya Marekani na Bahrain na pia utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ni makubwa sana na Washington inashiriki katika ukandamizaji dhidi ya wapinzani wa nchi hiyo ya Kiarabu." Baraka inazotoa Marekani kwa utawala wa Aal-Khalifa, ndizo zinazoufanya utawala huo uwe na jeuri zaidi ya kushadidisha jinai zake dhidi ya wanaharakati wa kisiasa wa Bahrain. Kwa kuzingatia kuwa utawala wa Manama daima umekuwa ukitumia mbinu za kiusalama katika kuamiliana na matakwa ya raia, hivyo ni wazi kuwa ukandamizaji ndio msingi mkuu wa hatua zinazochukuliwa na Aal Khalifa katika kukabiliana na wapinzani. Kwa kutumia ukandamizaji, Aal-Khalifa wanajaribu kuzima sauti ya malalamiko ya wananchi nchini, suala ambalo limeigeuza Bahrain kuwa jela na mahala pa utesaji raia.

Watawala wa Bahrain wanaopata amri na maelekezo kutoka Marekani

Kuhusiana na suala hilo, Jawad Abdul-Wahhab, mtaalamu wa masuala ya habari na siasa wa Bahrain anasema: "Fikra ya utawala wa Aal-Khalifa imejengeka juu ya utesaji na ukandamizaji kwa lengo la kuivunja irada ya wananchi na ili uweze kuzima vuguvugu la mapinduzi ya wananchi hao." Nukta ya kufaa kuzingatiwa katika ripoti hiyo mpya kuhusiana na ukiukaji wa haki za binaadamu nchini Bahrain ni kuzidi kuwa mbaya hali ya mambo nchini humo katika mwaka huu wa 2017 huku mashirika ya haki za binaadamu yakisisitiza kuwa, faili la haki za binaadamu la utawala wa Aal-Khalifa ni moja ya mafaili machafu na yenye madoa mengi zaidi duniani.