Wayemen waandamana kulaani ukatili wa Saudia dhidi yao
(last modified Sun, 27 Aug 2017 07:43:15 GMT )
Aug 27, 2017 07:43 UTC
  • Wayemen waandamana kulaani ukatili wa Saudia dhidi yao

Mamia ya maelfu ya wananchi wa Yemen kwa mara nyingine tena wamefanya maandamano katika mji mkuu Sana'a kulaani ukatili na mashambulizi ya kila uchao ya Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo maskini.

Katika maandamano hayo ya jana Jumamosi katika eneo la Faj Atan, viungani mwa mji wa Sana'a, waandamanaji  walisikika wakitoa nara dhidi ya umwagaji damu unaofanywa na Saudia nchini humo kwa zaidi ya miaka miwili sasa.

Mwanasheria Mkuu wa Yemen, Abdulaziz Al-Baghdadi, ambaye alikuwa miongoni mwa waandamanaji hao amesema: "Jinai hizo za Saudia dhidi ya Yemen zimefikia upeo wa juu haswa unapoona maiti za watoto wadogo zimetapakaa katika kila kona ya nchi." 

Hujuma za Saudia dhidi ya makazi ya raia Yemen

Makazi ya raia katika eneo la Faj Atan yalishambuliwa siku ya Ijumaa na ndege za muungano wa kijeshi unaoongozwa na utawala wa Aal-Saud na kuua raia 14 wakiwemo wanawake wawili na watoto sita, mbali na kujeruhi watu wengine 16.

Hii ni katika hali ambayo, Msemaji wa Kamishna wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Liz Throssel, Ijumaa iliyopita alisema kuwa, kati ya Agosti 17 na 24 pekee, raia 58 wameuawa nchini Yemen wakiwemo 42 waliouawa na muungano wa kijeshi wa utawala wa kifalme wa Aal-Saud.

Mashambulio ya anga yanayofanywa usiku na mchana na ndege za kivita za Saudi Arabia nchini Yemen yameshaua watu zaidi ya 13,000 hadi sasa, wakiwemo wanawake na watoto na kuwafanya wengine zaidi ya milioni tatu wabaki bila ya makaazi tangu utawala huo wa Aal Saud ulipoanzisha vita dhidi ya nchi hiyo mwezi Machi mwaka 2015.

Lengo la Riyadh ni kuisambaratisha harakati ya wananchi ya Ansarullah  na kumrejesha madarakani kibaraka wake aliyekuwa rais wa nchi hiyo Abd Rabbuh Mansur Hadi.