Wazayuni waandamana tena kulalamikia ufisadi wa Netanyahu
Kwa mara nyingine tena maelfu ya Wazayuni wamefanya maandamano katika mji wa Tel Aviv huko Israel kushinikiza kuuzuliwa Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala huo ghasibu wakimtuhumu kwa kujihusisha na vitendo vya ufisadi.
Katika maandamano hayo ya jana Jumamosi, Wazayuni wapatao 2,000 waliandamana na kukusanyika mbele ya nyumba ya Avichai Mendelblit, Mwanasheria Mkuu wa Israel wakilalamikia jinsi afisa huyo anavyoshughulikia faili la kesi ya ufisadi inayomkabili Netanyahu.
Waandamanaji hao waliokuwa wamebeba mabango na maberamu walisikika wakipiga nara za kulaani vitendo vya ufisadi vya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu. Aidha waandamanaji hao wamemtuhumu Mwanasheria Mkuu wa utawala haramu wa Israel kwamba, ni mshirika wa Benjamin Netanyahu na amekuwa akimkingia kifua kila mara anapokabiliwa na ghadhabu na malalamiko ya Wazayuni.
Maandamano haya yamefanyika chini ya wiki mbili baada ya mengine kufanyika viungani mwa mji wa Tel Aviv, kukosoa ufisadi wa Netanyahu.
Netanyahu na mkewe wanatuhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa baadhi ya mashirika makubwa ya kibiashara na vilevile kufanya mazungumzo na Arnon Mozes, mchapishaji na mmiliki mwenza wa gazeti la Yediot Ahronoth ili atangaze habari zinazompendelea kwa lengo la kulidhoofisha jarida pinzani la Israel, la Hayom.
Kabla ya kukabiliwa na kesi hii, Benjamin Netanyahu alishawahi kuhojiwa mara tatu huko nyuma kuhusu ufisadi wa fedha na kutumia vibaya madaraka.