UN yaitaka Israel iondoe mzingiro wa kibaguzi Ukanda wa Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i33811-un_yaitaka_israel_iondoe_mzingiro_wa_kibaguzi_ukanda_wa_gaza
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kusitishwa mzingiro wa kibaguzi wa karibu muongo mmoja dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 30, 2017 10:55 UTC
  • UN yaitaka Israel iondoe mzingiro wa kibaguzi Ukanda wa Gaza

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kusitishwa mzingiro wa kibaguzi wa karibu muongo mmoja dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Antonio Guterres ameyasema hayo leo Jumatano baada ya kuitembelea shule inayosimamiwa na Wakala wa Wakimbizi wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza UNRWA na kuongeza kuwa, hali ya Wapalestina wa eneo hilo ndio mbaya zaidi ya kibinadamu katika zama hizi.

Guterres amesema kuwa: "Nimeguswa sana kuwa Gaza hii leo, kwa masikitiko nimeshuhudia mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu ambao sijawahi kushuhudia katika miaka ya hivi karibuni katika shughuli zangu za masuala ya kibinadamu."

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye leo alikuwa anahitimisha safari yake ya siku tatu katika ardhi za Palestina zinakalowa kwa mabavu amesisitiza udharura wa kuondolewa mzingiro huo dhidi ya Gaza.

Uhaba wa maji kutokana na mzingiro Gaza

Tangu Januari mwaka 2006 na kufuatia ushindi wa harakati ya Hamas katika uchaguzi wa Bunge la Palestina, utawala wa Kizayuni wa Israel uliliwekea eneo la Ukanda wa Gaza mzingiro wa angani, baharini na nchi kavu kwa lengo la kuisambaratisha harakati hiyo ya muqawama.

Mzingiro huo unazuia kuingizwa katika eneo la Gaza bidhaa za mahitaji ya msingi zikiwemo za fueli, dawa na vifaa vya ujenzi.