Amnesty International yalaani ukiukwaji haki za binadamu nchini Bahrain
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema utawala wa Bahrain si tu kuwa hautekelezi ahadi zake kuhusu kulinda haki za binadamu bali pia uanendelea kutumia mkono wa chuma kukandamiza maandamano ya amani ya wanaotaka mabadiliko ya kisiasa nchini humo.
Katika taarifa mapema leo Alhamisi, Amnesty imeashiria kuteswa makumi ya wapinzani wa utawala wa kifalme nchini Bahrain. Imesema utawala wa Bahrain unapaswa kuchukua hatua za haraka na pasina masharti kuwaachilia huru wafungwa na kutokandamizwa maandamano ya amani nchini humo.
Aidha shirika hilo limetaka Bahrain ibatilishe uamuzi wake wa kupiga marufuku vyama viwili vikuu vya upinzani katika bunge la nchi hiyo. Amnesty pia imezikosoa Uingereza na Marekani kwa kuendelea kuunga mkono utawala wa kiimla wa Aal Khalifa nchini Bahrain ambao unaendelea kukandamiza wapinzani.
Tangu Februari 14 mwaka 2011, Bahrain imekuwa ikishuhudia vuguvugu la mapinduzi ya wananchi dhidi ya utawala kibaraka na wa kidikteta wa ukoo wa Aal Khalifa. Wananchi hao wanataka kuweko uhuru, uadilifu, kuondolewa ubaguzi na kuingia madarakani serikali ambayo imechaguliwa na wananchi wenyewe. Hatua zote za utawala huo za kuzima vuguvugu hilo hadi sasa hazijafanikiwa.