HAMAS: Hakuna cha kuzungumzwa kuhusu silaha za muqawama
Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesisitiza kwamba katika mazungumzo na harakati ya Fat-h, Hamas haikukubaliana na wazo la kuwapokonya silaha wanamuqawama na kwamba suala hilo halikujadiliwa katika mazungumzo yaliyopita wala halitojadiliwa katika mustakabali.
Musa Abu Marzouq, ambaye pia ni mwanachama mwandamizi wa Hamas ameliambia shirika la habari la Anatolia kwamba Hamas imepiga hatua za msingi mbele kwa ajili ya kuleta suluhu baina ya Wapalestina na imelegeza msimamo katika mambo mengi ili kupunguza mateso wanayopata watu wa Ukanda wa Gaza na kuweza kupatikana umoja katika safu za Wapalestina kwa ajili ya kupambana na uvamizi wa utawala wa Kizayuni wa Israel na Uyahudishaji wa Quds tukufu.
Kuhusu suala la kubadilishana mateka na utawala wa Kizayuni, Abu Marzouq amesema, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu ameiomba Russia, Misri, Uturuki, Qatar na nchi nyenginezo ziwe wapatanishi kati ya utawala huo na Hamas ili upatikane mwafaka mpya juu ya suala la ubadilishanaji mateka, lakini Hamas haitofanya mazungumzo yoyote mapya kabla ya kuachiwa huru kwanza mateka waliopita wa Palestina waliokamatwa tena na utawala wa Kizayuni baada ya kuachiwa huru.
Kiongozi huyo wa Hamas aidha ameuelezea uhusiano wa harakati hiyo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni mzuri na kusisitiza kwamba: Iran ni miongoni mwa waungaji mkono muhimu zaidi wa muqawama wa Palestina.../