Saudia yakasirishwa na ripoti ya UN kwamba inakiuka haki za binaadamu
Saudia imekasirishwa sana na ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa kwamba imehusika na jinai za kivita dhidi ya watoto wadogo nchini Yemen.
Umoja wa Mataifa umeiweka Saudia na nchi washirika wake katika orodha ya nchi watenda jinai za kivita dhidi ya watoto. Kwa mujibu wa ripoti, viongozi wa Riyadh wamesema kuwa, ripoti zinazoihusisha nchi hiyo na ukandamizaji wa haki za binaadamu ni zenye kuchukiza sana. Hii sio mara ya kwanza kwa mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binaadamu kuitaja Saudia kuwa mkandamizaji wa haki za binaadamu na mtenda jinai za kivita nchini Yemen.
Mwaka jana Umoja wa Mataifa uliiweka Saudia katika orodha nyeusi ya kutenda jinai za vita dhidi ya watoto nchini Yemen, hata hivyo Riyadh ilitumia lobi yake kubwa kuushinikiza umoja huo kuliondoa jina la Saudia katika orodha hiyo. Saudia kwa kushirikiana na Marekani, Imarati, Israel na baadhi ya nchi za Kiarabu na zisizo za Kiarabu, ilianzisha mashambulizi ya kila upande nchini Yemen kuanzia mwezi Machi mwaka 2015. Katika vita hivyo vilivyoandamana na mzingiro wa ardhini, angani na baharini dhidi ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu, zaidi ya watu elfu 12 wameuawa, maelfu ya wengine kujeruhiwa na mamilioni kuwa wakimbizi. Aidha mbali na hasara za kibinaadamu, hujuma hizo za Saudia zimesababisha uharibifu mkubwa kwa miundombinu ya nchi hiyo.