Israel yazitaka balozi zake kushirikiana zaidi na Saudia dhidi ya Hizbullah
Utawala haramu wa Kizayuni na katika kulinda maslahi ya Saudi Arabia duniani dhidi ya haraki ya Kiislamu ya Hizbullah ya nchini Lebanon, imetoa ujumbe kwa balozi zake kuhusiana na suala hilo.
Vyombo vya habari vya Israel Jumanne ya leo vimetangaza kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje ya utawala huo haramu sambamba na kutuma ujumbe kwa balozi zake katika mataifa mbalimbali, imezitaka kushirikiana zaidi na utawala wa Aal-Saud dhidi ya harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya nchini Lebanon.
Tangazo hilo ambalo ni uungaji mkono wa wazi wa Israel kwa Saudi Arabia dhidi ya Hizbullah, limetolewa katika hali ambayo Marekani imeiwekea vikwazo zaidi harakati hiyo ambayo imekuwa na nafasi muhimu katika kuyaangamiza makundi ya kigaidi nchini Syria na kuzuia njama za utawala haramu wa Israel. Aidha msimamo mpya wa utawala wa Kizayuni umetolewa huku Saad Hariri, Waziri Mkuu wa Lebabon Jumamosi iliyopita akitangaza kujiuzulu nafasi yake hiyo akiwa mjini Riyadh, ikiwa ni katika kutekeleza siasa za madola ya Magharibi na Kiarabu za kueneza chuki dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na muqawama. Katika tangazo hilo Hariri pia alitoa tuhuma nzito zisizo na ukweli kuilenga Tehran na harakati hiyo ya Kiislamu ya Hizbullah.
Duru za kisiasa nchini Lebanon zimemtaja Hariri kuwa mtekelezaji mkuu wa mpango wa pamoja wa Saudia dhidi ya muqawama kupitia kubuni tuhuma bandia zisizo na msingi dhidi ya Tehran na Hizbullah. Hivi karibuni pia afisa mmoja wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambaye hakutaka jina lake litajwe alifichua kuwa Muhammad bin Salman Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia mwezi Septemba mwaka huu alifanya safari za siri huko Israel ambapo alikutana na viongozi wa ngazi za juu wa Kizayuni.