Karzai: Marekani inashirikiana na ISIS (Daesh) nchini Afghanistan
Rais wa zamani wa Afghanistan, Hamid Karzai amesema Marekani inafanya kazi bega kwa bega na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) katika nchi hiyo inayoshuhudia vita na ukosefu wa uthabiti kwa miaka mingi sasa.
Katika mahojiano na kanali ya televisheni ya al-Jazeera ya Qatar, Karzai amesema kwa mtazamo wake, genge la kigaidi na kitaifiri la Daesh limechipuka na kuimarika nchini Afghanistan chini ya uwepo na uangalizi wa Marekani, kijeshi na kisiasa.
Amesema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, licha ya kilio cha Waafghani na mateso wanayopitia chini ya harakati za kundi hilo la ukufurishaji, lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na Marekani katika uwanja huo.
Kadhalika kwa mara nyingine tena Hamid Karzai amekosoa kitendo cha Marekani kuvurumisha bomu la "Mama wa Mabomu Yote" lenye uzito wa tani 11 za mada za milipuko ya TNT na lenye uharibifu mkubwa zaidi kuliko mabomu yote yasiyo ya nyuklia duniani katika mji wa Achin mkoa wa Nangarhar mwezi Aprili mwaka huu akisisitiza kuwa, Washington ilichukua hatua hiyo ya kufanyia majaribio silaha zake katika ardhi ya Afghanistan kwa kisingizio cha kulenga ngome ya ISIS.
Hivi karibuni, Rais huyo wa zamani wa Afghanistan, alisema kuwa Marekani ndiyo ilianzisha kundi la kigaidi la Daesh kwa ajili ya kufikia maslahi yake haramu katika eneo la Mashariki ya Kati, na kwamba hakuna tofauti baina ya Marekani na kundi hilo la kigaidi.