Hamas yatunisha misuli yake Ukanda wa Gaza
Wapiganaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas wamefanya mazoezi ya kijeshi katika eneo la Ukanda wa Gaza kwa shabaha ya kuzidisha utayarifu wao kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi ya aina yoyote ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Mazoezi hayo ya kijeshi yaliyoshirikisha maelfu ya wapiganaji wa Hamas yamefanyika sambambana na kutangazwa hali ya hatari kwa masaa kadhaa katika maeneo ya Bait Hanun, Bait Lahia na Jabalia huko kaskazini mwa Ukanda wa Gaza. Iyad Albazm ambaye ni miongoni mwa maafisa wa Palestina katika Ukanda wa Gaza amesema mazoezi hayo yamefanyika kwa mafanikio na kwamba kiwango cha utayarifu wa wapiganaji wa Hamas ni cha kuridhisha. Albazm amesisitiza kuwa, mazoezi makubwa ya Hamas yamewashirikisha wapiganaji elfu 15 na yamefanyika kwa lengo la kudhamini utayarifu wao wa kuingia kwenye medani wakati wa dharura katika siku za usoni.
Hali ya sasa ya Palestina imeathiriwa na kushindwa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel mbele ya mapambano ya Wapalestina katika Intifadha mpya ya Quds iliyoanza miezi kadhaa iliyopita. Katika mazingira hayo kufanyika kwa mazoezi ya kijeshi ya Hamas kwa ajili ya kutunisha misuli kumedhihirisha tena nguvu na uwezo wa wanamapambano hao mbele ya utawala katili wa Israel. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kuangamiza nguvu ya wanamapambano wa Palestina na kuharibu kabisa silaha zao ni miongoni mwa malengo makuu ya Israel katika mashambulizi yake ya mara kwa mara dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza lakini mazoezi hayo yamebatilisha propaganda hizo na kueonesha tena kwamba, kama ilivyokuwa huko nyuma, utawala huo umefeli katika mufikia malengo yake.
Mazoezi ya kutunisha misuli ya Hamas katika eneo la Gaza na uungaji mkono mkubwa wa wananchi kwa harakati hiyo vimeonesha tena kwamba mapambano ya Waislamu wa Palestina yanapata nguvu zaidi siku baada ya siku na kudhihirisha tena udhaifu wa Isarel katika medani za mapambano.
Kushindwa mara kwa mara utawala huo ghasibu mbele ya wanamapambano wa Palestina hususan katika vita vya Gaza katika miaka ya hivi karibuni kumebatilisha propaganda na madai ya kutoshindwa utawala huo ghasibu.
Hapana shaka kuwa wanamapambano wa Palestina wamewapa wananchi moyo na ari kubwa zaidi kwa kadiri kwamba Wapalestina wanautambua ushindi wa harakati kama Hamas kuwa ni mwanzo wa kukombolewa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina kutoka kwenye makucha ya Wazayuni maghasibu. Kwa msingi huo Wapalestina wanasisitiza kuwa, utawala ghasibu wa Israel utakabiliwa na kipigo kikali iwapo utaendelea kukiuka makubaliano ya kusitisha vita.
Alaa kulli hal mazoezi ya kijeshi na kutunisha misuli kwa wapiganaji wa Hamas katika Ukanda wa Gaza kunaonesha tena udhaifu wa Israel na kushindwa kwake kuangamiza mapambano ya Wapalestina kupitia njia ya vikwazo na mzingiro wa eneo hilo. Ikumbukwe kuwa tangu mwaka 2007 utawala bandia wa Israel uliwawekea mzingiro wa pande zote watu wa Ukanda wa Gaza kwa shabaha ya kuwazidishia mashinikizo na kutaka kuwalazimisha wasalimu amri mbele ya siasa za kikoloni za utawala huo. Hata hivyo kusimama kidete kwa Wapalestina hususan mashujaa wa Gaza kumezidi kuwakasirisha wazayuni wa Israel na kuwafanya washindwe la kufanya ghairi ya kutumia mbinu za kikatili zaidi kama kuchoma moto nyumba za raia na kuwateketeza wakiwa hai.
Matukio ya hivi karibuni ikiwa ni pamoja na kushindwa mara kwa mara kwa utawala wa Kizayuni mbele ya irada na azma ya wanapambano wa Kipalestina na vilevile kufeli kwa majaribio ya makombora na kuongezeka idadi ya askari wanaokimbia jeshi la Israel ni ishara kwamba mlingano wa nguvu katika eneo la Mashariki ya Kati unaunufaisha zaidi mrengo wa muqawama na mapambano.