Arab League yaionya Marekani dhidi ya kuuhamishia ubalozi wake Quds
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i37129-arab_league_yaionya_marekani_dhidi_ya_kuuhamishia_ubalozi_wake_quds
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imeonya kuwa, kuhamishiwa ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi mji mtukufu wa Quds hakutakuwa na natija nyingine ghairi ya kuibua ghasia na kuvuruga zaidi hali ya mambo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 03, 2017 10:56 UTC
  • Arab League yaionya Marekani dhidi ya kuuhamishia ubalozi wake Quds

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imeonya kuwa, kuhamishiwa ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi mji mtukufu wa Quds hakutakuwa na natija nyingine ghairi ya kuibua ghasia na kuvuruga zaidi hali ya mambo.

Ahmed Aboul Gheit, Katibu Mkuu wa Arab League amesema hatua hiyo itakuwa yenye maslahi kwa upande mmoja ambao hauthamini amani.

Amesema: "Jumuiya hii inaweka wazi kuwa, kitendo hicho cha kuhamishwa ubalozi wa Marekani hakitakuwa ni kwa maslahi ya amani na uthabiti katika eneo la Mashariki ya Kati, lakini kitakuwa ni sawa na kumwaga mafuta kwenye moto wa machafuko na ghasia ambazo tayari zinashuhudiwa."

Awali vyombo vya habari vilitangaza kuwa Rais Donald Trump wa Marekani anaazimia kuutambua rasmi mji mtakatifu wa Quds kuwa mji mkuu wa utawala ghasibu wa Israel na kuhamishia ubalozi wa nchi hiyo katika mji huo kutoka Tel Aviv.

Rais Trump wa Marekani

Kufuatia hatua hiyo ya Marekani, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepiga kura likipinga hatua yoyote ya kuutambua mji wa Quds ( Jerusalem) kuwa ni mji mkuu wa Israel. Nchi 151 wanachama wa baraza hilo zilitangaza Alkhamisi iliyopita kwamba mji huo hauna mfungamano wowote na utawala ghasibu wa Israel.  

Aidha, Nabil Abu Rudeina, msemaji wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amemuonya Trump dhidi ya kuhamishia ubalozi wa nchi hiyo katika mji mtakatifu wa Quds na kutambua rasmi kitendo cha kukaliwa kwa mabavu eneo hilo kama mji mkuu wa utawala haramu wa Israel, huku akisisitiza kuwa, utatuzi wowote wa mgogoro wa Mashariki ya Kati kati ya Palestina na utawala za Kizayuni wa Israel unalazimika kutambua rasmi Quds kama mji mkuu wa nchi huru ya Palestina.