Wapalestina walaani mpango wa kihaini wa mrithi wa ufalme wa Saudia
Wanaharakati wa Kiplaestina katika mitandao ya kijamii wamelaani mpango wa mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia wa kutatua kadhia ya Palestina.
Katika jibu na radiamali waliyotoa kwa mpango uliopendekezwa na Muhammad bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudia wa kubadilisha mji mkuu wa Palestina, wanaharakati hao wameulaani mpango huo na kusisitiza kuwa Baitul Muqaddas (Jerusalem) utabaki kuwa mji mkuu wa Palestina.
Gazeti la New York Times linalochapishwa nchini Marekani limezinukuu duru za Palestina na kuandika kuwa Muhammad bin Salman amependekeza kwa Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina mpango wenye manufaa kwa utawala wa Kizayuni tu wa Israel ambao ni mbaya zaidi kuliko hata ule wa Rais Donald Trump wa Marekani.
Kuna uwezekano hivi karibuni Trump atatangaza msimamo wa kuitambua rasmi Quds tukufu kuwa mji mkuu wa utawala bandia wa Israel. Wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais wa Marekani, Donald Trump aliahidi kuuhamishia Baitul Muqaddas ubalozi wa Marekani ulioko Tel Aviv.
Kwa mujibu wa New York Times, katika mpango aliopendekeza, Bin Salman ameigawa Palestina katika maeneo manne yatakayokuwa na mamlaka ya kujiendeshea mambo yao sambamba na kutaka vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni vilivyoko katika Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan viendelee kuwa milki ya utawala haramu wa Israel.
Mpango huo wa kihaini wa mrithi wa ufalme wa Saudia umependekeza mji wa Abu Dis uwe ndio mji mkuu wa Palestina badala ya Baitul Muqaddas Mashariki inayokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni. Aidha wakimbizi wa Kipalestina hawatokuwa na haki ya kurudi kwenye ardhi zao za asili.../