Hamas yasema kesho ni 'Ijumaa ya Ghadhabu' ya kuihami Quds
(last modified Thu, 07 Dec 2017 14:50:18 GMT )
Dec 07, 2017 14:50 UTC
  • Hamas yasema kesho ni 'Ijumaa ya Ghadhabu' ya kuihami Quds

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas imeutaja uamuzi wa Rais wa Marekani, Donald Trump wa kuitangaza Baytul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel kama tangazo la vita huku ikisema kuwa kesho itakuwa Ijumaa ya Ghadhabu na fursa kwa ulimwengu wa Kiislamu kuonyesha hasira zao dhidi ya Washington na Tel Aviv.

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas, Ismail Haniya ametoa mwito wa kuanza Intifadha mpya kuanzia kesho Ijumaa huku akikitaja kitendo hicho cha Trump kama 'uvamizi dhidi ya Waislamu' na 'vita dhidi ya matukufu ya Kiislamu'.

Katika hotuba aliyoitoa hii leo kupitia televisheni, Haniya amesema, na hapa tunanukuu: "Sera ya Kizayuni kwa baraka na uungaji mkono wa Marekani haiwezi kusambaratishwa isipokuwa kwa kuanzisha Intifadha, mwamko na mapambano mapya kuanzia kesho Ijumaa." Mwisho wa kunukuu.

Amesema Quds Tukufu ni milki ya Waarabu na Waislamu wote na ni mji mkuu wa Palestina, huku akimtaka Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kujiepusha na jitihada zozote za eti amani na Israel. Aidha amezitaka nchi za Kiarabu kuususia utawala wa Trump.

Maandamano ya Wapalestina Ukanda wa Gaza

Wakati huo huo, viongozi wa ngazi za juu wa harakati ya Jihad Islami wamesisitizia udharura wa Wapalestina wote kuungana na kuweka pembeni tofauti zao kwa shabaha ya kupambana na uvamizi mpya na chokochoko za Israel. 

Haya yanajiri katika hali ambayo, maandamano yanaendelea katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Ukanda wa Gaza na katika nchi kama Jordan na Lebanon kulalamikia uamuzi huo wa rais wa Marekani wa kuutangaza mji wa Quds ambao ni Kibla cha kwanza cha Waislamu kuwa eti ni mji mkuu wa Israel.

Tags