Hizbullah: Mapambano ndio njia pekee ya Wapalestina kupata ushindi
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, hatua ya Rais wa Marekani ya kuutangaza mji wa Baytul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel, utakuwa ni msukumo kwa watu waliokuwa kando, lakini kwa sasa wanapaswa kuingia katika medani bila ya kisingizio chochote.
Katika hotuba yake ya jana, Donald Trump alidai kuwa, suala la kuitangaza Quds kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni ilibidi lifanyike miaka mingi nyuma na kwamba serikali yake imechukua uamuzi huo ambao umewashinda marais wote waliotangulia wa Marekani.
Sheikh Naim Qassim amesema hayo katika kikao cha Muungano wa Kimataifa wa Maulama wa Muqawama uliofanyika pambizoni mwa Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu mjini Tehran ambapo ameashiria nafasi na mchango wa muqawama na mapambno ya Kiislamu katika nchi mbalimbali na kusema kuwa, kambi ya muqawama inasimama kidete katika medani mbalimbali kwa ajili ya kukabiliana na njama tofauti za maadui.
Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, kambi ya muqawama ilifanikiwa kupata ushindi mwaka 1993, 1996 na 2006 na hivi sasa ushindi mtawalia wa kambi ya muqawama unashuhudiwa katika nchi mbalimbali.
Sheikh Naim Qassim amebainisha kwamba, kambi ya muqawama ikipata uungaji mkono wa Iran imefanikiwa kupata ushindi mwaka huu dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh ambalo lilianzishwa na kupewa misaada na Marekani na utawala ghasibu wa Israel.
Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, eneo la Ukanda wa Gaza lisingefikia ushindi wa sasa kama si kuwa na kambi ya muqawama na kwamba, kila nchi inayofuata muqawama huungwa mkono, na kuwa ushindi wa nchi za muqawama umezifurahisha nchi zote za Kiislamu.