Trump, Quds inayokaliwa kwa mabavu na sheria za kimataifa
Tukiachilia mbali kujadili ni matokeo gani hasi na mabaya utakuwa nayo uamuzi aliochukua Donald Trump kuitangaza Baitul Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni, kuuhakiki uamuzi huo katika mtazamo wa sheria za kimataifa kuna umuhimu mkubwa.
Uamuzi aliochukua Donald Trump unaweza kuelezewa kuwa ni hatua inayokinzana waziwazi na sheria za kimataifa na nidhamu iliyobuniwa na Marekani yenyewe ambayo ndiyo inayotawala katika mfumo wa dunia hivi sasa. Ukweli wa mambo ni kwamba Marekani ilikuwa na nafasi kuu katika kuasisi mfumo unaotawala sasa duniani; lakini rais wa sasa wa nchi hiyo hakubaliani kwa kiwango kikubwa hata na mfumo ulioasisiwa na Marekani yenyewe. Kuhusiana na nukta hiyo tahariri ya toleo la siku ya Alkhamisi ya tarehe 7 Desemba la gazeti la Le Monde linalochapishwa nchini Ufaransa imeeleza kuhusiana na uamuzi uliochukuliwa na Trump kuhusu mji wa Quds, kwamba kiongozi huyo hajakomea hapo kwa kujichukulia maamuzi ya upande mmoja yanayokinzana na mtazamo wa washirika wake wa karibu mno, lakini ukweli ni kwamba: "Marekani imeufuta mfumo wa uhusiano wa kimataifa ambao yenyewe ndiyo iliyouanzisha baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia".
Suala jengine ni kwamba kwa uamuzi aliochukua, Donald Trump amekiuka na kupuuza kanuni za kimataifa zilizorasimishwa kuhusiana na Quds inayokaliwa kwa mabavu, yakiwemo maazimio ya Baraza Kuu na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Baada ya vita vya mwaka 1967, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio nambari 242 linaloeleza kwamba, kwa mtazamo wa kisheria, maeneo yaliyovamiwa na utawala wa Kizayuni katika vita hivyo, yanayojumuisha miinuko ya Golan ya Syria, Ukanda wa Gaza na Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan ambao unajumuisha ndani yake eneo la Baitul Muqaddas Mashariki, ni maeneo yanayokaliwa kwa mabavu; na kwa muktadha huo Israel inalazimika kuondoka kwenye maeneo hayo. Hata hivyo hadi sasa sio tu utawala wa Kizayuni wa Israel haujaondoka kwenye maeneo hayo ya ardhi za Palestina unayoyakalia kwa mabavu, lakini kama vile haitoshi, Trump amelikiuka azimio hilo la Umoja wa Mataifa na kuamua kuutunukia utawala huo ghasibu mji wa Baitul Muqaddas, mahali kilipo kibla cha kwanza cha Waislamu.
Hata katika miaka ya hivi karibuni pia, Baraza Kuu na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yamepitisha maazimio mengine kadhaa ambayo kwa uchache yametangaza kuwa eneo la Baitul Muqaddas Mashariki ni milki ya Wapalestina. Kuhusiana na jambo hilo, mnamo mwezi Novemba mwaka 2015, yalipitishwa maazimio sita dhidi ya Israel katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambapo katika moja ya maazimio hayo mataifa ya dunia yalitangaza rasmi kuwa ujenzi wa vitongoji unaofanywa na Israel katika ardhi za Palestina ni haramu na kinyume cha sheria. Aidha yalieleza wasiwasi yalionao kuhusu hatua yoyote inayochukuliwa na Israel ikiwemo kuwawekea vizuizi na mipaka Wapalestina ya kuingia na kutoka kwenye mji wa Baitul Muqadda na kuutenganisha mji huo na maeneo mengine ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Lakini pia yakasisitiza kupitia azimio hilo kwamba hatua zote zinazochukuliwa na Israel kuhusiana na Baitul Muqaddas ni kinyume cha sheria na hazina itibari yoyote.

Inapasa tubainishe pia kwamba uamuzi aliochukua Trump ni ukiukaji wa wazi wa azimio nambari 2231 lililopitishwa mwezi Desemba mwaka uliopita wa 2016 na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kulaani ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni. Kwa uamuzi wake huo, sio tu Trump ametoa kibali kwa Israel cha kujenga vitongoji vyengine vipya katika Quds inayokaliwa kwa mabavu, -ambapo mara tu baada ya kutangazwa uamuzi huo wa rais wa Marekani, baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni lilipitisha mpango wa ujenzi wa nyumba nyengine mpya 14,000 katika mji wa Baitul Muqaddas- lakini kimsingi hasa ni kwamba ameutangaza ujenzi wa vitongoji kuwa ni hatua halali na ya kisheria inayochukuliwa na Israel.
Tahariri ya gazeti la Le Monde linalochapishwa nchini Ufaransa imeuzungumzia tena uamuzi wa Rais wa Marekani kwa kuandika: "katika hotuba yake, Trump amesema ni "hali halisi" Quds kuwa mji mkuu wa Israel na wala hakuashiria chochote na kwa namna yoyote ile kwamba Quds ya Mashariki ni mji mkuu wa Palestina. Kwa mantiki hii, sheria za kimataifa zinakiukwa, na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu unatafsiriwa kuwa ni "hali halisi". Tahariri hiyo ya gazeti la Le Monde inamalizia kwa kusema: "inaonekana wazi kwamba katika sera za nje za Trump, sheria za kimataifa hazina nafasi yoyote".../