Erdogan: Israel ni dola vamizi na la kigaidi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i37565-erdogan_israel_ni_dola_vamizi_na_la_kigaidi
Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesema kuwa, kuwa na nguvu na kumiliki silaha si dalili kuwa Marekani ina nguvu, na maamuzi yake yatasababisha matatizo makubwa katika eneo la Mashariki ya Kati.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 13, 2017 16:13 UTC
  • Erdogan: Israel ni dola vamizi na la kigaidi

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesema kuwa, kuwa na nguvu na kumiliki silaha si dalili kuwa Marekani ina nguvu, na maamuzi yake yatasababisha matatizo makubwa katika eneo la Mashariki ya Kati.

Erdoğan ambaye alikuwa akizungumza leo katika ufunguzi wa kikao cha dharura cha viongozi wa nchi wanachama katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kilichoanza leo mjini Istanbul huko Uturuki amesema uamuzi uliochukuliwa na Rais Donald Trump wa Marekani wa kuutangaza mji mtakatifu wa Quds (Jerusalem) kuwa ni mji mkuu wa Israel unakiuka sheria zote na utasababisha matatizo makubwa.

Ameongeza kuwa, Israel inajenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi iliyoghusubiwa ya Palestina na kuwafukuza Wapalestina katika makazi na nyumba zao, kuwaua na kufanya mashambulizi ya kigaidi lakini Marekani inaendelea kuipongeza kwa kuipa tuzo na zawadi.

Rais wa Uturuki ameongeza kuwa, hapana shaka kwamba nchi wanachama katika Umoja wa Mataifa zitapinga uamuzi huo wa Marekani kuhusu mji mtukufu wa Quds unaokaliwa kwa mabavu na Israel.

Erdogan katika mkutano wa OIC

Erdoğan amehoji kwa kwa kusema: Tukwambie nini ewe Trump, na tukuthibitishe vipi kwamba Israel ni dola vamizi na la kigaidi ili upate kulipa tuzo kwa vitendo vyake viovu?

Rais wa Uturuki amesisitiza kuwa, Israel ni dola vamizi na la kigaidi na kwamba Waislamu hawatakubali kugawanywa Quds tukufu.

Vilevile ameashiria jinsi wanajeshi wa Israel wanavyowakamata watoto wadogo wenye umri wa miaka kumi wa Palestina na kuwafungia katika matundu ya chuma na amezishukuru nchi zote zilizopinga uamuzi batili wa Marekani kuhusu mji wa Quds (Jerusalem) ambao haukuungwa mkono isipokuwa na utawala ghasibu wa Israel.

Mkutano wa OIC, Istanbul

Mkutano wa siku mbili wa  viongozi wa nchi za Kiislamu umeanza leo huko Uturuki na ajenda yake kuu ni Quds tukufu na uamuzi wa Marekani wa kuutambua mji huo mtakatifu unaokaliwa kwa mabavu kuwa ni mji mkuu wa utawala haramu wa Israel.