Hamas: Hakuna nchi inayoitwa 'Israel' hata mji mkuu wake uwe 'Quds'
(last modified Thu, 14 Dec 2017 16:01:52 GMT )
Dec 14, 2017 16:01 UTC
  • Hamas: Hakuna nchi inayoitwa 'Israel' hata mji mkuu wake uwe 'Quds'

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas imelaani vikali uamuzi wa Rais wa Marekani, Donald Trump wa kuitangaza Baytul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel na kusisitiza kuwa, hakuna dola linaloitwa Israel hata mji mkuu wake uwe Quds tukufu.

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas, Ismail Haniya ameyasema hayo leo katika mji wa Gaza, kwa mnasaba wa kutimia miaka 30 tangu kuasisiwa kwa harakati hiyo ya mapambano.

Amesema Hamas iliundwa kwa shabaha ya kuihami Quds tukufu na Palestina kwa ujumla na kubainisha kwamba, wapenda haki kote duniani wanaunga mkono kadhia ya Palestina.

Afisa huyo wa ngazi za juu wa Hamas ameashiria juu ya maandamano yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika katika pembe mbali mbali za dunia, kupinga kitendo hicho cha Trump akisisitiza kuwa, hakuna dola lolote duniani lenye mamlaka na uwezo wa kubadilisha utambulisho wa Baitul Muqaddas.

Maelfu washiriki maadhimisho ya miaka 30 tangu kuasisiwa Hamas, huko Gaza

Ismail Haniya amesema: "Kuna haja ya kuundwa muungano wenye nguvu katika eneo la Mashariki ya Kati utakaotetea suala la Palestina. Lazima Intifadha iendelee. Kila Ijumaa inapaswa kuwa 'Ijumaa ya Ghadhabu' ya kulaani uvamizi na ukaliaji wa mabavu  wa ardhi za Wapalestina unaofanywa na Israel."

Kadhalika Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas amewataka Waislamu na Wakristo kote duniani kushirikiana katika kulinda maeneo matukufu katika mji wa Quds ambao anasema ni wa dunia yote.

Nchi, serikali na asasi mbali mbali kote duniani zimeonyesha kughadhibishwa na chokochoko hiyo mpya ya Marekani ya kuitambua Quds kuwa mji mkuu wa utawala vamizi wa Israel, huku taarifa ya mwisho ya mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ikisisitiza kutambuliwa rasmi serikali ya Palestina ambayo mji mkuu wake ni Quds Mashariki (Jerusalem).

Tags