Safari ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i3796-safari_ya_katibu_mkuu_wa_umoja_wa_mataifa_nchini_lebanon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amesisitizia ulazima wa kuongezwa misaada ya kimataifa kwa jeshi la Lebanon.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 25, 2016 21:10 UTC
  • Safari ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amesisitizia ulazima wa kuongezwa misaada ya kimataifa kwa jeshi la Lebanon.

Ban Ki-moon aliyasema hayo siku ya Alkhamisi alipokutana na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa nchini Lebanon (UNIFIL) katika makao makuu ya vikosi hivyo kwenye eneo la Naqoura, kusini mwa Lebanon. Amesema ili amani na uthabiti upatikane kusini mwa Lebanon kuna ulazima kwa pande zote husika kusimamisha harakati za kivita. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa kuongeza na kuimarisha uwezo wa vikosi vya ulinzi vya Lebanon ndiko kunakodhamini usalama wa nchi hiyo na ndilo suala la msingi la kufanikisha kazi za UNIFIL.

Kikosi cha kwanza cha askari na maafisa wa UNIFIL kiliwasili eneo la kusini mwa Lebanon tarehe 23 Machi mwaka 1978 baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kuvamia na kulikalia kwa mabavu eneo hilo.

Askari hao walitumwa kusini mwa Lebanon kwa mujibu wa maazimio nambari 425 na 426 ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kwenda kushuhudia kuondoka kwa jeshi la Israel katika eneo hilo na wakati huo huo kuisaidia serikali ya Lebanon ili iweze kulinda mamlaka yake ya utawala. Hata hivyo wakati jeshi la utawala haramu wa Israel lilipovamia tena kusini mwa Lebanon mnamo mwaka 1982, vikosi vya Umoja wa Mataifa vilishughulika zaidi na kazi ya ufikishaji misaada kwa wananchi walioathiriwa na vita; na badala ya kutekeleza jukumu lake la ulinzi vilibaki kuwa mtazamaji tu wa uvamizi na jinai zilizokuwa zikifanywa na jeshi la Kizayuni.

Matukio ya Lebanon yameonyesha kuwa njia pekee ya kudhamini kinga na ulinzi wa kuzuia chokochoko za utawala wa Kizayuni na tishio la makundi ya ukufurishaji ni kuimarisha mihimili ya ulinzi ya nchi hiyo, ambayo ni jeshi na muqawama wa wananchi.

Kila mara Lebanon imekuwa ikishuhudia ukiukwaji wa mipaka yake ya angani, baharini na nchi kavu unaofanywa na utawala wa Kizayuni; na katika miaka ya karibuni, makundi ya kigaidi ya Daesh na Jabhatun-Nusra yamekuwa tatizo sugu kwa Lebanon katika mpaka wake wa pamoja na Syria.

Katika hali hiyo, kushirikiana bega kwa bega vikosi vya muqawama na jeshi kumewezesha kila mara kuzima njama za maadui wa ndani na nje dhidi ya Lebanon.

Sisitizo la fikra za waliowengi na maafisa wa Umoja wa Mataifa juu ya kuimarishwa uwezo wa kiulinzi na kijeshi wa Lebanon kwa ajili ya kukabiliana na vitisho vinavyoongezeka dhidi ya nchi hiyo linatolewa katika hali ambayo kuna harakati za kutia shaka zinazofanywa na maadui wa Lebanon kwa lengo la kudhoofisha uwezo wa kujilinda na wa kukabiliana na vitisho vinavyoikabili. Harakati hizo zinaashiria njama hatari inayopangwa na kutekelezwa dhidi ya Lebanon na utawala wa Kizayuni ukishirikiana na baadhi ya nchi za Magharibi zinazouunga mkono utawala huo pamoja na baadhi ya nchi za Kiarabu.

Saudi Arabia ndiye mtekelezaji mkuu wa njama hiyo, ambapo katika miezi ya hivi karibuni tumeshuhudia harakati kadhaa za utawala wa Aal Saud dhidi ya Lebanon. Kukataa utawala huo kuipatia serikali ya Beirut msaada wa kijeshi uliouahidi, sambamba na propaganda na tuhuma za Saudia dhidi ya harakati ya muqawama wa Kiislamu ya Lebanon Hizbullah, yote hayo yanaweza kutathminiwa katika muelekeo wa utekelezaji wa njama hiyo.

Kwa muda wa miaka kadhaa, Lebanon imeziomba Marekani na nchi za Ulaya msaada wa silaha za kisasa ili kulijenga na kulizatiti jeshi lake, lakini hadi sasa nchi hizo zimekataa kufanya hivyo kwa sababu ya kudhamini malengo ya utawala wa Kizayuni.

Hakuna shaka yoyote kuwa harakati na hatua hizo za nchi za Magharibi na Saudi Arabia zimezusha wimbi la malalamiko ya fikra za waliowengi; na sisitizo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ulazima wa kuimarishwa vikosi vya ulinzi vya Lebanon lina maana ya kupinga umoja huo njama zozote za kuidhoofisha nchi hiyo.../