Palestina: Uamuzi wa Guatemala kuuhamishia ubalozi wake Quds ni 'fedheha'
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i38123-palestina_uamuzi_wa_guatemala_kuuhamishia_ubalozi_wake_quds_ni_'fedheha'
Palestina imekosoa vikali hatua ya Guatemala ya kuuhamishia ubalozi wake Quds Tukufu kutoka Tel Aviv na kukitaja kitendo hicho kama 'fedheha'.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 26, 2017 07:30 UTC
  • Palestina: Uamuzi wa Guatemala kuuhamishia ubalozi wake Quds ni 'fedheha'

Palestina imekosoa vikali hatua ya Guatemala ya kuuhamishia ubalozi wake Quds Tukufu kutoka Tel Aviv na kukitaja kitendo hicho kama 'fedheha'.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imesema hatua hiyo ya serikali ya Guatemala ya kupuuza azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa juu ya mji huo mtukufu ni jambo la kufedhehesha na kinyume cha sheria.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: Taifa la Palestina linaitazama hatua hiyo kama ya kiuhasama na inayokanyaga haki za Wapalestina na sheria za kimataifa. Palestina itashirikiana na washirika wake kieneo na kimataifa kupinga uamuzi huo ulio kinyume cha sheria.

Rais wa Guatemala, Jimmy Morales

Taarifa hii ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imetolewa siku moja baada ya Rais Jimmy Morales wa Guatemala kutangaza kuwa nchi hiyo ndogo ya Amerika ya Kati atauhamishia Quds (Jerusalem) ubalozi wa nchi hiyo ulioko Tel Aviv, ikiwa ni nchi ya kwanza kufuata kibubusa nyayo za Rais Donald Trump wa Marekani.

Disemba 6, Trump alitangaza kuwa eti Quds ni mji mkuu wa utawala haramu wa Israel, hatua ambayo imepingwa na kulaaniwa vikali na aghlabu ya nchi duniani na taasisi za kimataifa likiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Baraza la Kuu la umoja huo.