Dec 27, 2017 02:41 UTC
  • Kuuawa watoto; mhimili wa jinai za Saudi Arabia nchini Yemen

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umeashiria maafa makubwa ya vita vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen na kuipa hujuma hiyo ya kijeshi ya Aal Saud jina la "Vita Dhidi ya Watoto".

Hadi hivi sasa zaidi ya watu 14 elfu wameshauawa na makumi ya maelfu ya wengine kujeruhiwa katika mashambulizi ya kivamizi yaliyoanzishwa na Saudi Arabia na kundi lake mwezi Machi 2015 dhidi ya taifa maskini la Yemen. Aidha mamilioni ya watu wamekuwa wakimbizi huku watoto wakiwa ndio wahanga wakuu wa jinai hiyo. Abdallah Shaaban, mwanaharakati wa kupinga mzingiro dhidi ya Yemen anasema kuhusiana na suala hilo kwamba: Mtoto mmoja wa Kiyemen huaga dunia kila baada ya dakika kumi kutokana na maradhi mbalimbali.

Saudi Arabia ambayo ni dhihirisho la Uwahabi na muenezaji wa itikadi potofu za kitakfiri na kisalafi kwa kuwauwa watoto imeonyesha kuwa,  haina mpaka wowote katika kutenda jinai na kwa kushadidisha jinai zake hizo inataka kuthibitisha utambulisho wake wa utumiaji mabavu. Utendaji huu ni kama utumiaji mabavu wa Kinazi, Ufashisti na Uzayuni katika uga wa mahusiano ya kimataifa. Licha ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF kukiri wazi juu ya matokeo mabaya ya mashambulio ya anga ya muungano unaoongozwa na Saudia dhidi ya raia wa Yemen hususan watoto, Umoja wa Mataifa si tu kwamba, haujachukua hatua yoyote ya maana ya kuhitimisha mashambulio hayo, bali hadi sasa Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo halijaunda tume huru ya kimataifa kwa ajili ya kuchunguza jinai za Wasaudia. 

Huduma za afya Yemen ni duni

Hivi karibuni Uholanzi ikiziwakilisha nchi kadhaa za Ulaya ilipendekeza mpango wa kuundwa kamati ya kimataifa ya kuchunguza jinai za Saudia huko Yemen ambapo utawala wa Riyadh ukipata uungaji mkono wa Marekani na Uingereza uliuzuia mpango huo. Kabla ya hapo pia, Umoja wa Mataifa ulitoa ripoti ambayo iliiweka Saudia katika orodha nyeusi ya nchi zenye kukiuka haki za watoto kutokana na kushambulia kwa mabomu shule na hospitali za Yemen.

Ripoti hiyo ilieleza kwamba, muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia huko Yemen unabeba dhima ya vifo vya watoto na majeruhi wa nchi hiyo mwaka uliopita. Hata hivyo baada ya siku chache tu tangu kutolewa ripoti hiyo, Ban Ki-moon aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo alilitoa jina la Saudia katika orodha hiyo nyeusi ya nchi zinazokanyaga na kukiuka haki za watoto kwa hoja kuwa, Riyadh ilitishia kwamba, kama jina lake halingeondolewa katika orodha ya nchi hizo zinazokiuka haki za watoto, ingekatisha misaada take ya kifedha kwa umoja huo.

Licha ya kuwa, katika kipindi cha uongozi wa Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa yaani Antonio Guterres, Saudia imewekwa tena katika orodha hiyo nyeusi kufuatia mashinikizo ya fikra za waliowengi, lakini katika kipindi hiki pia hakujachukuliwa hatua au kutekelezwa mashinikizo yoyote dhidi ya nchi hiyo. Mambo yanaendelea kama vile hakuna jinai yoyote iliyofanywa na Saudia.

Maandamano ya kulaani jinai za Saudia huko Yemen

Muamala na utendaji huu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na jinai za Saudi Arabia huko Yemen, unaonyesha kuwa,  taasisi hiyo imegeuzwa na kuwa klabu ya matajiri na watu wenye ushawishi ambapo jambo muhimu kuliko yote ni kulindwa maslahi yao. Kama ambavyo Umoja wa Mataifa haukuchukua hatua yoyote dhidi ya utawala vamizi wa Israel ambao ulifanya mashambulio mtawalia katika maeneo ya Wapalestina ukiwemo Ukanda wa Gaza na kufanya mauaji ya maelfu ya raia wakiwemo watoto wadogo.

Kwa hakika uungaji mkono huu ndio ambao licha ya kutolewa indhari nyingi na baadhi ya asasi na makundi katika Umoja wa Mataifa kuhusiana na hali mbaya ya kibinadamu, umepelekea indhari hizo kutokuwa na dhamana ya kufanyiwa kazi. Kiujumla Umoja wa Mataifa si tu kwamba, haujatekeleza jukumu lake la kulinda amani na usalama wa kimataifa, bali misimamo yake ya kindumakuwili na ya upande mmoja imechangia kuendelea jinai za Saudia dhidi ya watu wa Yemen hususan watoto wadogo.

 

Tags