Unduli wa Israel wa kutaka kuua Wapalestina wengi zaidi
Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni ametaka kunyongwa raia wa Palestina kufuatia kushtadi wimbi la malalamiko ya raia hao.
Avigdor Lieberman amesisitiza juu ya udharura wa kupasishwa sheria ya kuwanyonga Wapalestina na huku akiashiria kuwepo sheria kama hiyo huko Marekani ameeleza kuwa: Ni vyema Israel pia ifuate mkondo huo wa Marekani kuhusiana na suala hilo.
Viongozi wa vyama vya muungano wa pande sita wa utawala wa Kizayuni siku kadhaa zilizopita waliafiki mpango ambao iwapo utaidhinishwa katika kikao cha bunge la utawala huo (Knesset); basi raia wa Palestina wanaopinga na kudhihirisha malalamiko yao watanyongwa. Kwa mujibu wa mpango huo eti wa kiusalama, Israel itakuwa na uwezo wa kutekeleza hukumu ya kunyonga kwa kuzingatia mamlaka ilizo nazo mahakama za kijeshi za utawala huo dhalimu. Hatua hiyo ya utawala wa Kizayuni imekumbwa na wimbi kubwa la malalamiko ya kupinga Uzayuni na Marekani kutoka kwa vijana wa Kipalestina. Baada ya rais wa Marekani, Donald Trump, kuchukua uamuzi wa kuitangaza Quds kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni; maeneo mbalimbali katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na Ukanda wa Ghaza hadi hivi sasa yanashuhudia maandamano ya Wapalestina ya kupiga hatua hiyo ya Trump sambamba na kujiri mapigano baina ya Wazayuni na raia wa Palestina. Wimbi jipya la malalamiko na upinzani wa Wapalestina chini ya anwani " Intifadha ya Tatu" limeutia wahka mkubwa utawala wa Kizayuni na Marekani.
Utawala wa Kizayuni chini ya baraka zote za Washington sambamba na kustafidi na tajiriba ya Marekani ambayo ina historia kubwa katika kuyakandamiza mataifa mbalimbali na kuendesha vitendo vya kibaguzi dhidi ya raia wake, hivi sasa umejielekeza katika kuandaa muongozo na ramani ya njia ya kuwakandamiza zaidi wananchi wa Palestina. Israel inachukua hatua za kupasisha sheria za kuwauwa zaidi wananchi wa Palestina katika fremu ya njama za pamoja za Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina. Mienendo hiyo ya kiwendawazimu ya utawala wa Kizayuni imedhihirisha wazi jinai dhidi ya binadamu na maangamizi ya kizazi yanayofanywa na Israel. Kuongezeka jinai za Israel katika miaka ya hivi karibuni kumechefua mioyo ya walimwengu.
Kenneth O'Keefe, mwanaharakati anayepinga vita wa nchini Marekani anasisitiza kuwa, jinai zinazofanywa na utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina ni matokeo ya fikra za kibaguzi za Kizayuni. Aidha anasema, Palestina iko katika kitovu cha udhalimu wote. Mwanaharati huyo anayepinga vita wa nchini Marekani ameongeza kuwa, Wapalestina wanaendelea kukandamizwa na utawala wa Kizayuni na madola ya Magharibi yanayouunga mkono utawala huo.
Kuendelea vitendo vya ukandamizaji na utumiaji mabavu vya utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Palestina umewafanya walimwengu watambue vyema na kutilia maanani sura halisi iliyo iliyo dhidi ya ubinadamu ya utawala huo dhalimu. Takwimu na ripoti mpya zilizotolewa kuhusu ukandamizaji wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina zinaonyesha kujiri maafa ya kutisha yaliyofanywa katika siku ya hivi karibuni katika duru mpya ya machafuko na utumiaji mabavu wa utawala huo dhidi ya wananchi madhlumu wa Palestina. Raia wa Palestina wanaendelea kukabiliwa na jinai za Israel; na utawala wa Kizayuni katika duru hii mpya ya ukandamizaji wake dhidi ya Wapalestina ambayo inahesabiwa kuwa ni siasa za siku zote za utawala huo dhidi ya raia hao, umekusudia kutekeleza mauaji zaidi ya Wapalestina kwa kutumia mbinu mbalimbali za kijinai kama kuwauwa kwa kuwanyonga Wapalestina wanaopinga ukaliaji mabavu wa utawala huo.