Arab League: Sharti Quds itambulike kimataifa kama mji mkuu wa Palestina
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imesema karibuni hivi itaanzisha jitihada za kuhakikisha kuwa Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kwa ujumla inalitambua taifa la Palestina, mji mkuu wake ukiwa Quds Tukufu.
Ayman Safadi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan amesema kuna haja Umoja wa Mataifa kuitambua Palestina kwa mujibu wa mipaka ya kimataifa ya mwaka 1967.
Safadi aliyasema hayo jana Jumamosi katika mji mkuu wa nchi hiyo Amman, kwenye mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Arab League.
Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Ahmed Aboul Gheit amesema jumuiya hiyo itaandaa msururu wa mikakati ya kuhakikisha kuwa uamuzi wa kisiasa katika duru za kimataifa wa kutambuliwa taifa la Palestina unafikiwa.
Itakumbukwa kuwa tarehe 6 Disemba mwaka jana, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza Quds Tukufu kuwa eti ni mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel na kueleza kuwa atauhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Quds.
Chokochoko hiyo ya Trump iliibua ghadhabu na malalamiko sio tu katika ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu, bali kote duniani.