Wapalestina wavuruga warsha ya Marekani Ukingo wa Magharibi
Wapalestina wenye ghadhabu wamevuruga warsha ya biashara iliyoandaliwa na Marekani katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Wapalestina wamechukua hatua hiyo ili kulalamikia hatua za kihasama za Rais Donald Trump wa Marekani dhidi yao. Habari zinasema kuwa, gari la mwanadiplomasia wa Marekani huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu limeharibiwa na waandamanaji hao katika vurumai hizo za jana Jumanne.
Samir Hazboun, mkurugenzi wa Jumuiya ya Biashara ya Bethlehem amesema ubalozi mdogo wa Marekani huko Quds Tukufu (Jerusalem) ndio ulioratibu warsha hiyo.
Wapalestina hao wamesema ni kinaya kwa Wamarekani kujifanya wanaandaa warsha ya kibiashara kwa maslahi ya Wapalestina, wakati ambapo wamechukua hatua nyingi za kihasama dhidi yao.
Rais wa Marekani hivi karibuni alitishia kuwa ataikatia misaada ya kifedha Mamlaka ya Ndani ya Palestina iwapo haitaonyesha nia ya kutaka kufikiwa makubaliano ya amani na Israel.
Kabla ya hapo, Trump alitangaza Quds Tukufu kuwa eti ni mji mkuu wa utawala pandikizi wa Israel na akatoa amri ya kufanyika taratibu za kuuhamishia mjini humo ubalozi wa Marekani ulioko Tel Aviv, mji mkuu wa utawala dhalimu wa Kizayuni.