UNICEF: Watoto milioni 11 wa Yemen wanahitajia misaada ya kibinadamu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i39719-unicef_watoto_milioni_11_wa_yemen_wanahitajia_misaada_ya_kibinadamu
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umetangaza kuwa, hali ya kibinadamu nchini Yemen ni mbaya mno na kwamba, zaidi ya watoto milioni 11 wa nchi hiyo wanahitajia misaada ya kibinadamu.
(last modified 2025-11-16T06:33:27+00:00 )
Jan 31, 2018 08:02 UTC
  • UNICEF: Watoto milioni 11 wa Yemen wanahitajia misaada ya kibinadamu

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umetangaza kuwa, hali ya kibinadamu nchini Yemen ni mbaya mno na kwamba, zaidi ya watoto milioni 11 wa nchi hiyo wanahitajia misaada ya kibinadamu.

Taarifa ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF imeeleza kwamba, hali ya kibinadamu nchini Yemen ni ya kutia wasiwasi mno hivyo kuna haja ya kuchukuliwa hatua za haraka kuwasaidia wananchi wa nchi hiyo.

UNICEF aidha imesema kuwa, huduma muhimu kama maji safi na salama ya kunywa hayapatikani na kwamba, zaidi ya watoto milioni moja wa nchi hiyo wana dalili za maradhi ya kipindupindu.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza wasiwasi wake kuhusu hali inayozidi kuwa mbaya ya watu wa Yemen.

Saudi Arabia imeendelea kufanya jinai dhidi ya Yemen licha ya malalmiko ya walimwengu

Antonio Guterres amesema kuwa kusimamisha mapigano na mivutano huko Yemen ndiyo njia bora zaidi kwa ajili ya kukabiliana na maafa ya kibinadamu yanayoisibu nchi hiyo kwa sasa.

Saudi Arabia mwezi Machi mwaka 2015 ilianzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu ikiungwa mkono na Marekani na ikaiwekea nchi hiyo mzingiro wa baharini, anga, na nchi kavu.

Makumi ya maelfu ya watu wameuawa hadi sasa tangu Saudi Arabia ianzishe uvamizi wake wa kijeshi huko Yemen na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi.