Feb 02, 2018 08:02 UTC
  • Askari kadhaa wa Saudia waangamizwa mkoani Jizan kusini mwa nchi hiyo

Askari kadhaa wa Saudi Arabia wameangamizwa katika shambulio lililofanywa na mdunguzi mmoja wa Yemen dhidi ya ngome za askari hao huko kusini mwa Saudia.

Kanali ya televisheni ya Al Masirah ya Yemen imeripoti kuwa mdunguzi huyo wa jeshi la Yemen jana alifanikiwa kuwalenga shabaha na kuwaua askari watano wa utawala vamizi wa Aal Saud katika mkoa wa Jizan huko kusini mwa Saudia.

Siku ya Jumatano pia askari watatu wa Saudi Arabia waliangamizwa katika shambulio la kuvizia lililofanywa na jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Yemen katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo wa Jizan.

Katika mwaka uliopita wa 2017 wadunguzi wa jeshi la Yemen na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa nchi hiyo walifanikiwa kuwalenga shabaha na kuwaangamiza jumla ya askari 49 wa Saudi Arabia pamoja na mamluki 296 wa utawala huo wa kifalme.

Mdunguzi wa vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Yemen

Katika kipindi hicho, jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Yemen viliyashambulia pia mara 45 kwa makombora maeneo mbalimbali ya ardhi ya Saudia.

Tangu mwezi Machi mwaka 2015, na kwa msaada na uungaji mkono wa Marekani, Saudi Arabia na waitifaki wake imeanzisha mashambulio ya kijeshi dhidi ya Yemen, sambamba na kuiwekea mzingiro wa angani, baharini na nchi kavu. Makumi ya maelfu ya Wayemeni wameuawa na makumi ya melfu ya wengine wamejeruhiwa hadi sasa huku mamilioni ya wengine wakipoteza makazi na kulazimika kuwa wakimbizi kutokana na moto wa vita uliowashwa na Saudia na waitifaki wake.../

 

Tags