Malenga wanne Saudia wafungwa miaka 30 jela kwa kumkosoa Bin Salman
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i39855-malenga_wanne_saudia_wafungwa_miaka_30_jela_kwa_kumkosoa_bin_salman
Mahakama ya Saudia imewahukumu kifungo cha miaka 30 jela wakosoaji wa Mohammad Bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 03, 2018 04:41 UTC
  • Malenga wanne Saudia wafungwa miaka 30 jela kwa kumkosoa Bin Salman

Mahakama ya Saudia imewahukumu kifungo cha miaka 30 jela wakosoaji wa Mohammad Bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa nchi hiyo.

Sambamba na kuongezeka kwa wimbi la kamatakamata dhidi ya wasomi wa kidini, wafanyabiashara, wanawafalme, wasomi na waandishi mbalimbali nchini Saudia, mara hii malenga wanne wa miji ya Tabuk na Ta'if, ambao walisoma kasida ya kumkosoa Bin Salman, wamehukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela. 

Mohammad Bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia ambaye hataki kukosolewa

Abdullah Atqan Salami na Muhammad Eid al-Hawiti, wamehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela kila mmoja huku Munif al-Munqarah na Sultan al-Shaibani al-Atibi wakihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kila mmoja. Shirika la Kutetea Haki za Binaadamu nchini Saudia al-Qist limekosoa vikali hukumu hiyo nzito dhidi ya malenga hao kwa tuhuma eti za uchochezi dhidi ya Mwanamfalme Bin Salman na washauri wake. Kabla ya hapo gazeti la Washington Post lilizitaja hatua za Mrithi huyo wa Kiti cha Ufalme kuwahusu raia wa Saudia kuwa za kujionyesha na kuandika kuwa, madai yake ya kupambana na ufisadi wa kifedha sambamba na siasa za kupunguza bajeti nchini, ni mambo yanayoenda kinyume na hatua yake ya kununua jumba la kifahari la mamia ya mamilioni ya Dola nchini Ufaransa na kadhalika ununuzi wa meli moja ya thamani ya Dola milioni 550.

Jumba la kifahari alilolinunua Bin Salman nchini Ufaransa kwa mamia ya mamilioni ya Dola

Kwa mujibu wa gazeti hilo, mambo hayo yanabainisha kuwepo propaganda katika siasa zake za kuwa huru raia wa nchi hiyo. Inaelezwa kuwa zaidi ya watu 200 wakiwemo wanawafalme, wafanyabiashara na viongozi wa zamani wa ngazi za juu serikalini na mawaziri, wametiwa mbaroni tangu mwezi Novemba mwaka jana na kuzuiliwa katika hoteli ya Ritz-Carlton, kabla ya wengine kuhamishiwa katika jela ya al-Ha'ir.