Saudia inawahudumia bure Wazayuni
Sheikh Suhail Habli, mwanazoni wa Kisuni wa nchini Lebanon amezikosoa siasa za watawala wa Aal Saud na kusema kuwa, Saudi Arabia ni mfanyakazi wa bure wa Wazayuni.
Sheikh Suhail amesisitiza kuwa, Saudia imekuwa ikiuhudumia bure utawala wa Kizayuni wa Israel unaotenda jinai kila siku iendayo kwa Mungu dhidi ya wananchi madhlumu wa Palestuna.
Mwanazuoni huyo wa Kisuni amelaani vikali hatua ya Saudia na viongozi wa Kiarabu wa Ghuba ya Uajemi ya kuiweka harakati ya Hizbullah ya Lebanon katika orodha ya makundi ya kigaidi na kusisitiza kwamba, hatua hiyo ni huduma ya bure kwa Wazayuni. Sheikh Suhail Habli ameitaja Saudia kuwa ni mshirika wa wazi wa ugaidi na kubainisha kwamba, huduma nzuri na ya bure ya Saudia kwa Israel inatolewa katika hali ambayo, Wazayuni hawajaacha kutumia njia yoyote ile kwa ajili ya kutoa pigo kwa Lebanon na muqawama wa wananchi wa nchi hiyo.
Kwa upande wake Sheikh Hassan Izzudeen Afisa Mahusiano wa Hizbullah ya Lebanin amesema kuwa, hatua ya Saudia ya kuiweka Hizbullah katika orodha eti ya makundi ya kigaidi inahudumia mipango michafu ya Israel katika Mashariki ya Kati.
Itakumbukwa kuwa, mwanzoni mwa mwezi huu Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi liliiweka harakati ya Hizbullah ya Lebanon katika orodha ya makundi ya kigaidi na kutangaza kuwa, limechukua hatua kadhaa katika uwanja huo. Hatua ya baraza hilo linaloundwa na nchi za Saudi Arabia, Qatar, Kuwait, Oman, Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain imekabiliwa na upinzani mkubwa ndani na nje ya Lebanon. Asasi na harakati mbalimbali za kieneo na kimataifa zimelaani vikali hatua hiyo ya Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi.