Safari yenye malengo ya uchaguzi ya Rais wa Misri nchini Imarati
(last modified Thu, 08 Feb 2018 07:53:40 GMT )
Feb 08, 2018 07:53 UTC
  • Safari yenye malengo ya uchaguzi ya Rais wa Misri nchini Imarati

Rais Abdul-Fatah al-Sisi wa Misri Jumanne ya juzi aliwasili Abu Dhabi katika mji mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) baada ya kukamilisha safari yake ya siku tatu huko Oman.

Mara baada ya kuwasili mjini humo, Rais al-Sisi alilakiwa na Muhammad bin Rashid al-Maktoum mtawala wa Dubai pamoja na Muhammad bin Zayed al-Nahyan mrithi wa kiti cha ufalme wa Abu Dhabi. Inawezekana kusema kuwa, Imarati ni moja ya nchi ambazo Jenerali al-Sisi amezitembelea sana tangu aliposhika hatamu za uongozi wa Rais nchini Misri. Moja ya sababu za jambo hilo ni kuwa, kinyume na uhusiano wa Cairo na Riyadh, uhusiano kati ya Abu Dhabi na Cairo umekumbwa mara chache sana na mivutano na una kiwango fulani cha uthabiti.

Moja kati ya mambo yaliyopelekea kuzorota kidogo uhusiano wa Misri na Imarati katika miaka ya hivi karibuni ni safari ya Aprili mwaka 2016 ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Uturuki nchini Imarati.

Kwa kuzingatia kwamba, Uturuki iliitaja hatua ya kuondolewa madarakni Rais Muhammad Mursi mwaka 2013 kuwa ni mapinduzi ya kijeshi, Misri haikutaraji kuiona Abu Dhabi ikipanua ushirikiano wake na Ankara. Pamoja na hayo, mvutano huo haukupanuka sana na ulikuwa wa muda tu.

Safari ya Rais al-Sisi nchini Oman

Imarati au Umoja wa Falme za Kiarabu ni miongoni mwa nchi ambazo ziliunga mkono mapinduzi ya kijeshi nchini Misri mwaka 2013 yaliyopelekea kuondolewa madarakani Rais halali na aliyechaguliwa kidemokrasia wa nchi hiyo Muhammad Mursi. Si hayo tu, bali serikali ya Imarati, Saudi Arabia na Kuwait katika mwaka huo wa 2013 na miaka ya baadaye ziliipatia msaada wa mabilioni ya dola serikali ya Misri.

Aidha serikali ya Imarati ikiwa na lengo la kuunga mkono mapinduzi ya kijeshi ya Misri, mwaka 2014 iliitangaza Harakati ya Ikwanul-Muslimin kuwa ni kundi la kigaidi. Kinyume na serikali ya Qatar ambayo iliunga mkono uwepo wa wanachama wa Ikhwanul-Muslimin katika nchi hiyo, serikali ya Abu Dhabi ikiwa pamoja na Cairo iliwatia mbaroni viongozi wa harakati hiyo waliokuwa nchini Imarati. Kwa muktadha huo, upinzani wa pamoja wa Cairo na Abu Dhabi dhidi ya Ikhwanul-Muslimin ni moja ya sababu za uhusiano wa nchi mbili hizo kuchukua mkondo wa kuimarika.

Rais wa Misri akifanya mazungumzo na mrithi wa kiti cha ufalme wa Abu Dhabi

Katika mazingira ya hivi sasa pia, kukabiliana kwa pamoja Misri na Imarati dhidi ya Qatar ni moja ya sababu za kuimarika uhusiano wa nchi mbili hizo. Misri pamoja na nchi tatu za Imarati, Saudi Arabia na Bahrain, Juni mwaka jana zilikata uhusiano wao na Qatar kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuunga mkono ugaidi Doha na hatua yake ya kutekeleza siasa ambazo ziko kinyume na eneo hilo.

Safari ya hivi sasa ya Jenerali Abdul-Fattah al-Sisi huko Abu Dhabu ni safari ya pili ya kiongozi huyo katika nchi hiyo tangu ulipoibuka mgogoro miongoni mwa nchi za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi Juni mwaka jana.

Safari ya kwanza ya Rais al-Sisi nchini Imarati baada ya mgogoro huo ilikuwa Septemba mwaka jana. Moja ya ajenda kuu za mazungumzo ya Rais wa Misri na viongozi wa Imarati ni mvutano ulioibuka miongoni mwa nchi za Kiarabu na namna ya kukabiliana na Qatar. 

Rais Abdul-Fattah al-Sisi wa Misri

Hapana shaka kuwa, moja ya sababu za safari ya Jenerali Abdul-Fattah al-Sisi huko Imarati ni kadhia ya uchaguzi ujao wa Rais nchini Misri uliopangwa kufanyika tarehe 28 mwezi ujao wa Machi.

Serikali ya Imarati si tu kwamba, iliisaidia kifedha serikali ya muda ya Misri baada ya mapinduzi dhidi ya Rais Mursi bali katika miaka iliyofuata pia iliendelea kuisaidia kifedha Cairo.

Hivi sasa pia ambapo Rais al-Sisi anajiandaa kushiriki katika kinyang'anyiro cha Urais mwezi ujao wa Machi, anataraji serikali ya Imarati itampatia uungaji mkono wa kifedha na usio wa kifedha. Kwa minajili hiyo basi, tunapaswa kusema kuwa, kabla ya mambo mengine suala la uchaguzi ndilo jambo lenye umuhimu kwa Rais Abdul-Fattah al-Sisi katika safari yake nchini Imarati.

Tags