Wakuu wa Iran, Ansarullah wajadili suluhisho la kisiasa Yemen, utoaji misaada
Maafisa wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Harakati ya Ansarullah ya Yemen wamefanya mazungumzo mjini Tehran kujadili njia za kuhitimisha mgogoro wa kisiasa katika nchi hiyo ya Kiarabu na udharura wa kuwaikifhsia misaada wananchi wake.
Siku ya Jumatatu, Hussein Jaberi Ansari, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayesimamia masuala ya kisiasa alikutana na kufanya mazungumzo na Mohammad Abdusalam, msemaji wa harakati ya Ansarullah.
Wawili hao walijadili njia za kuwafikishia misaada ya dharura wananchi wa Yemen ambao wamekuwa wakiandamwa na hujuma za kinyama za Saudia na waitifaki wake tokea Machi 2015. Aidha walijadili njia za kutafuta suluhisho la kisiasa la mgogoro wa Yemen.
Abdusalam aliwasili katika mji mkuu wa Iran Jumamosi ambapo alifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje Mohammad Javad Zarif. Alimkabidhi Zarif ripoti ya hali ya mambo nchini Yemen. Katika kikao hicho Zarif aliashiria mpango wa hatua nne alioupendekeza wa kumaliza mgogoro wa Yemen huku akisisitiza ulazima wa kusimamishwa mara moja hujuma na mzingiro wa Saudia dhdii ya watu wa Yemen sambamba na kurahisishwa ufikishaji misaada kwa wanaohitaji.