Ban ailaani tena Israel kwa kughusubu ardhi za Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i406-ban_ailaani_tena_israel_kwa_kughusubu_ardhi_za_palestina
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kwa mara nyingine ameulaani utawala wa Israel kwa hatua yake ya kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina na kujenga vitongoji vya Wazayuni kinyume cha sheria katika ardhi hizo zilizoghuhusubiwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 02, 2016 00:16 UTC
  • Ban ailaani tena Israel kwa kughusubu ardhi za Palestina

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kwa mara nyingine ameulaani utawala wa Israel kwa hatua yake ya kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina na kujenga vitongoji vya Wazayuni kinyume cha sheria katika ardhi hizo zilizoghuhusubiwa.

Katika makala aliyoliandikia gazeti la New York Times Jumatatu ya jana, Ban amesema ,"Historia imethibitisha kuwa watu daima watapambana dhidi ya kukaliwa kwa mabavu ardhi zao."

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani pia mpango wa Israel wa kujenga vitongoji vipya na kunyakua ekari 370 za ardhi za kilimo za Palestina katika eneo inalolikalia kwa mabavu la Ukingo wa Magharibi. Amesema kupuuza dhulma ambazo Israel inawatendea Wapalestina hakuwezi kupelekea tatizo hilo kutoweka.

Katika siku za hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekuwa akieleza upinzani wake mkali kuhusu sera za Israel. Janauri 26 wmaka huu akihutubu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon alisema Israel inapaswa kusitisha ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ili kupigwe hatua kuelekea kwenye amani. Siku iliyofuata, Ban alihutubia Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za Wapalestina na kusema, Wapalestina, hasa vijana wanapoteza matumaini na wamekasirishwa na sera za ukandamizaji wa utawala ghasibu wa Israel. Kauli hiyo ilipelekea Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni kudai kuwa Umoja wa Mataifa unapendelea upande moja. Katika kujibu matamshi hayo ya Netanyahu, Ban Ki-moon aliandika makala katika jarida la Times chini ya anwani: "Israel, Mjumbe Hauawi."

Zaidi ya Waisraeli nusu milioni wanaishi katika vitongoji 230 haramu vilivyojengwa katika ardhi za Palestina zilizoghusubiwa mwaka 1967 katika Ukingo wa Magharibi na Quds Mashariki.