Sheikh wa al-Aqsa aonya kuhusu huhamishiwa Quds ubalozi wa US
Mhubiri mtajika wa Msikiti wa al-Aqsa, Sheikh Ikrima Sabri ametahadharisha kuhusu azma ya Marekani ya kuuhamishia ubalozi wake mjini Quds Tukufu kutoka Tel Aviv na kuitaja hatua hiyo kama ya kichokozi na kichochezi.
Sheikh Ikrima Sabri ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu wa Baitul Muqaddas (Jerusalem) amesema kitendo hicho cha Marekani hakina nia nyingine ghairi ya kuamsha ghadhabu za Waislamu na kuzusha migogoro zaidi katika eneo.
Katika mahojiano na shirika la habari la Tasnim, mwanachuoni huyo amesema Marekani, Uingereza na Ufaransa zinauunga mkono na kuukingia kifua utawala wa Kizayuni wa Israel, ili kutia woga kwenye nyoyo za Waislamu.
Ijumaa iliyopita, Heather Nauert, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alitangaza azma ya nchi hiyo kuhamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv, mji mkuu wa utawala haramu wa Israel kwenda mji wa Quds, tarehe 14 Mei mwaka huu.
Itakumbukwa kuwa, Mei 14 itasadifiana na Siku ya Nakba, inayokumbushia tukio la kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina na utawala ghasibu wa Israel.
Hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuitangaza Quds Tukufu (Jerusalem) kuwa mji mkuu wa Israel iliibua makelele na malalamiko mengi katika kona zote za dunia.